Job 3

Hotuba Ya Kwanza Ya Ayubu

Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake.

Akasema: “Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali,
nao usiku ule iliposemekana,
‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’
Siku ile na iwe giza,
Mungu juu na asiiangalie,
nayo nuru isiiangazie.
Giza na kivuli kikuu kiikalie tena,
wingu na likae juu yake,
weusi na uifunike nuru yake.
Usiku ule na ushikwe na giza kuu,
usihesabiwe katika siku za mwaka,
wala usihesabiwe katika siku
za mwezi wo wote.
Usiku ule na uwe tasa,
sauti ya furaha na isisikike ndani yake.
Wale wazilaanio siku, wailaani hiyo siku,
wale walio tayari
kumwamsha Lewiathani
3.8 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa
.
Nyota zake za alfajiri na ziwe giza,
nao ungojee mwanga bila mafanikio,
wala usiuone muonzi wa kwanza
wa mapambazuko,
10 kwa sababu huo usiku haukunifungia
mlango wa tumbo la mama yangu,
ili kuyaficha macho yangu
kutokana na taabu.
11 “Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa?
Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni?
12 Kwa nini pakawa na magoti ya kunipokea
na matiti ili nipate kunyonyeshwa?
13 Kwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani,
ningekuwa nimelala na kupumzika
14 pamoja na wafalme na washauri wa dunia,
waliojijengea kwa ajili yao mahali
ambapo sasa ni magofu,
15 pamoja na watawala waliokuwa na dhahabu,
waliozijaza nyumba zao kwa fedha.
16 Au kwa nini sikufichwa ardhini
kama mtoto aliyezaliwa mfu,
kama mtoto mchanga ambaye
kamwe hakuuona mwanga?
17 Huko waovu huacha kusumbua
na huko waliochoka hupumzika.
18 Wafungwa nao hufurahia utulivu wao,
hawasikii tena sauti ya kukemea
ya kiongozi wa watumwa.
19 Wadogo na wakubwa wamo humo,
na mtumwa ameachiwa huru
kutoka kwa bwana wake.
20 “Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni
na hao wenye uchungu kupewa uhai?
21 Kwa nini wale wanaotamani kufa hilo haliji,
wale watafutao kufa
zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa,
22 ambao hujawa na furaha
na shangwe wafikapo kaburini?
23 Kwa nini uhai hupewa mtu
ambaye njia yake imefichika,
ambaye Mungu amemzungushia boma?
24 Kwa maana kulia kwangu kwa uchungu
kwanijia badala ya chakula;
mlio wangu wa kusononeka
unamwagika kama maji.
25 Lile nililokuwa naliogopa limenijia;
lile nililokuwa ninalihofia limenipata.
26 Sina amani, wala utulivu;
sina pumziko, bali taabu tu.”


Copyright information for Neno