Job 32

SEHEMU YA TATU: MAZUNGUMZO YA ELIHU

Elihu Awakemea Rafiki Za Ayubu

Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe. Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu amejihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu. Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu. Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kuliko yeye. Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka.

Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema: “Mimi ni mdogo kwa umri,
nanyi ni wazee;
ndiyo sababu niliogopa,
sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua.
Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme,
nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’
Lakini ni Roho iliyoko ndani ya mwanadamu,
pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo yeye ufahamu.
Sio wazee peke yao walio na hekima,
wala sio wenye umri mkubwa peke yao
wanaofahamu lililo sawa.
10 “Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni mimi;
mimi nami nitawaambia lile ninalojua.
11 Nilingojea mlipokuwa mnaongea,
nilizisikiliza hoja zenu,
mlipokuwa mkitafuta maneno ya kusema,
12 niliwasikiliza kwa makini.
Lakini hakuna hata mmoja wenu
aliyethibitisha kwamba Ayubu amekosa,
wala hakuna hata mmoja wenu
aliyeweza kujibu hoja zake.
13 Msiseme, ‘Tumepata hekima,
Mungu na amthibitishe kuwa mwongo,
wala si mwanadamu.’
14 Lakini Ayubu hajayapanga maneno yake dhidi yangu,
nami sitamjibu kwa kutumia hoja zenu.
15 “Wametiwa hofu na hawana la zaidi la kusema,
maneno yamewaishia.
16 Je, ningoje sasa kwa sababu wamekuwa kimya,
kwa vile sasa wanasimama bila kuwa na la kujibu?
17 Mimi nami nitakuwa na la kusema,
mimi nami nitasema lile nilijualo.
18 Kwa kuwa nimejawa na maneno,
nayo Roho iliyomo ndani yangu yanisukuma,
19 ndani yangu niko kama chupa iliyojazwa divai,
kama kiriba kipya cha divai kilicho tayari kupasuka.
20 Ni lazima niseme ili niweze kutulia,
ni lazima nifumbue midomo yangu nipate kujibu.
21 Sitampendelea mtu ye yote,
wala sitajipendekeza kwa mtu ye yote,
22 kwa kuwa kama ningekuwa stadi wa kujipendekeza,
Muumba wangu angeniondolea mbali kwa upesi.


Copyright information for Neno