Job 40

1BWANA akamwambia Ayubu: 2“Je, mwenye kushindana na Mwenyezi aweza kumsahihisha?
Mwenye kumlaumu Mungu na ajibu.”3Ndipo Ayubu akamjibu BWANA: 4“Mimi sistahili kabisa, ninawezaje kukujibu wewe?
Nauweka mkono wangu juu ya kinywa changu.
5Nimesema mara moja, lakini sina jibu;
naam, nimesema mara mbili,
lakini sitasema tena.”6Ndipo BWANA akasema na Ayubu kutoka katika upepo wa kisulisuli: 7“Jikaze kama mwanaume;
nitakuuliza maswali, nawe yakupasa unijibu.
8“Je, utabatilisha hukumu yangu?
Utanilaumu mimi ili kujihesabia haki mwenyewe?
9Je, una mkono kama wa Mungu,
nawe waweza kutoa sauti ya ngurumo kama yake?
10Basi jivike mwenyewe utukufu na fahari,
nawe uvae heshima na enzi.
11Fungulia ukali wa ghadhabu yako,
mtafute kila mwenye kiburi umshushe,
12mwangalie kila mtu mwenye kiburi na umnyenyekeze,
waponde waovu mahali wasimamapo.
13Wazike wote mavumbini pamoja,
wafunge nyuso zao kaburini.
14Ndipo mimi mwenyewe nitakukubalia kuwa
mkono wako mwenyewe wa kuume unaweza kukuokoa.
15“Mwangalie kiboko, niliyemwumba kama nilivyokuumba wewe,
ambaye anajilisha kwa majani kama ng'ombe.
16Tazama basi, nguvu alizo nazo kwenye viuno vyake,
uwezo alio nao kwenye misuli ya tumbo lake!
17Mkia wake hutikisika kama mwerezi,
mishipa ya mapaja yake imesukwa pamoja.
18Mifupa yake ni bomba za shaba,
maungo yake ni kama fito za chuma.
19Yeye ni wa kwanza miongoni mwa kazi za Mungu,
lakini Muumba wake anaweza
kumsogelea kwa upanga wake.
20Vilima humletea yeye mazao yake,
nao wanyama wote wa porini hucheza karibu naye.
21Hulala chini ya mimea ya yungiyungi,
katika maficho ya matete kwenye matope.
22Hiyo mimea ya yungiyungi humficha kwenye vivuli vyake;
miti mirefu karibu na kijito humzunguka.
23Wakati mto ufurikapo, yeye hapati mshtuko wa hofu;
yeye yu salama, hata kama Yordani
ingefurika hadi kwenye kinywa chake.
24Je, mtu ye yote anaweza kumkamata yeye akiwa macho,
au kumnasa kwa mtego na kutoboa pua yake?


Copyright information for Neno