Job 41

1“Je, waweza kumvua Lewiathani
41.1 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa
kwa ndoano ya samaki
au kufunga ulimi wake kwa kamba?
2Waweza kupitisha kamba puani mwake
au kutoboa taya lake kwa kulabu?
3Je, ataendelea kukuomba umhurumie?
Atasema nawe maneno ya upole?
4Je, atafanya agano nawe ili umtwae
awe mtumishi wako maisha yake yote?
5Je, utamfuga na kumfanya rafiki kama ndege,
au kumfunga kamba kwa ajili ya wasichana wako?
6Je, wafanya biashara watabadilishana bidhaa kwa ajili yake?
Watamgawanya miongoni mwa wafanyao biashara?
7Je, waweza kuijaza ngozi yake kwa vyuma vyenye ncha kali,
au kichwa chake kwa mkuki wa kuvulia samaki?
8Kama ukiweka mkono wako juu yake,
utavikumbuka hivyo vita na kamwe hutarudia tena!
9Tumaini lo lote la kumtiisha ni kujidanganya,
kule kumwona tu kunamwangusha mtu chini.
10Hakuna ye yote aliye mkali athubutuye kumchokoza.
Ni nani basi awezaye kusimama dhidi yangu Mimi?
11Ni nani mwenye madai dhidi yangu ili nipate kumlipa?
Kila kitu kilicho chini ya mbingu ni mali yangu.
12“Sitashindwa kunena juu ya maungo yake,
nguvu zake na umbo lake zuri.
13Ni nani awezaye kumvua gamba lake la nje?
Ni nani awezaye kumsogelea na lijamu?
14Nani athubutuye kuufungua mlango wa kinywa chake,
kilichozungukwa na meno yake ya kutisha pande zote?
15Mgongo wake una safu za ngao
zilizoshikamanishwa imara pamoja,
16kila moja i karibu sana na mwenzake
wala hakuna hewa iwezayo kupita kati yake.
17Zimeunganishwa imara kila moja na nyingine,
zimeng'ang'aniana pamoja
wala haziwezi kutenganishwa.
18Akipiga chafya mwanga humetameta,
macho yake ni kama mionzi ya mapambazuko.
19Mienge iwakayo humiminika kutoka kinywani mwake,
cheche za moto huruka nje.
20Moshi hufuka kutoka puani mwake,
kama kutoka kwenye chungu
kinachotokota kwa moto wa matete.
21Pumzi yake huwasha makaa ya mawe,
nayo miali ya moto huruka kutoka kinywani mwake.
22Nguvu hukaa katika shingo yake,
utisho hutangulia mbele yake.
23Mikunjo ya nyama yake imeshikamana imara pamoja,
iko imara na haiwezi kuondolewa.
24Kifua chake ni kigumu kama mwamba,
kigumu kama jiwe la chini la kusagia.
25Ainukapo, wenye nguvu wanaogopa,
wenye nguvu hurudi nyuma mbele yake
anapokwenda kwa kishindo.
26Upanga unaomfikia haumdhuru,
wala mkuki au mshale wala fumo.
27Chuma hukiona kama unyasi
na shaba kama mti uliooza.
28Mishale haimfanyi yeye akimbie;
mawe ya kombeo kwake ni kama makapi.
29Rungu kwake huwa kama kipande cha jani kavu;
hucheka sauti za kugongana kwa mkuki.
30Sehemu zake za chini kwenye tumbo
zina menomeno na mapengo kama vigae vya chungu,
zikiacha mburuzo kwenye matope
kama chombo chenye meno cha kupuria.
31Huvisukasuka vilindi kama sufuria kubwa ichemkayo
na kukoroga bahari kama chungu cha marhamu.
32Anapopita nyuma yake huacha mkondo unaometameta;
mtu angedhani vilindi vilikuwa na mvi.
33Hakuna cho chote duniani kinacholingana naye,
kiumbe kisicho na woga.
34Yeye huwatazama chini wale wote wenye kujivuna;
yeye ni mfalme juu ya wale wote wenye kiburi.”
Copyright information for Neno