John 10

Mchungaji Mwema

1“Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, ni mwivi na mnyang'anyi. 2Yeye anayeingia kwa kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo. 3Mlinzi humfungulia lango na kondoo huisikia sauti yake. Huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi. 4Akiisha kuwatoa wote nje, hutangulia mbele yao na kondoo humfuata kwa kuwa wanaijua sauti yake. 5Lakini kondoo hawatamfuata mgeni bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.” 6Yesu alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia.

7Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. 8Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi, lakini kondoo hawakuwasikia. 9Mimi ndimi lango, ye yote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho. 10Mwivi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.

11“Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. 12Mtu wa kuajiriwa ambaye kondoo si mali yake, amwonapo mbwa mwitu anakuja, hukimbia na kuwaacha kondoo na mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. 13Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.

14“Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. 15Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. 17Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. 18Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”

19Kwa maneno haya Wayahudi waligawanyika. 20Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.”

21Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu mwenye pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”

Yesu Akataliwa Na Wayahudi

22Wakati huo ilikuwa Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu,
10.22 Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu ni Hanukkah kwa Kiebrania
nao ulikuwa wakati wa majira ya baridi.
23Naye Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika ukumbi wa Solomoni. 24Wayahudi wakamkusanyikia wakamwuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo
10:24 Yaani Masiya
tuambie waziwazi.”

25Yesu akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia. 26Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu. 27Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata, 28nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka katika mikono yangu. 29Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake. 30Mimi na Baba yangu tu umoja.”

31Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo, 32lakini Yesu akawaambia, “Nimewaonyesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni ipi katika hiyo mnataka kunipiga mawe?”

33Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ingawa ni mwanadamu unajifanya kuwa Mungu.”

34Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Torati ya kwamba, ‘Nimesema kuwa, ninyi ndinyi miungu?’ 35Kama aliwaita ‘miungu,’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka. 36Je, mwawezaje kusema kwamba, yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru kwa sababu nilisema ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’ 37Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini, 38lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ndani yake.” 39Ndipo wakajaribu kumkamata kwa mara nyingine, lakini akaponyoka kutoka mikononi mwao.

40Akaenda tena ng'ambo ya Mto Yordani mpaka mahali pale ambapo Yohana alikuwa akibatiza hapo awali, naye akakaa huko. 41Watu wengi wakamjia, nao wakawa wakisema, “Yohana hakufanya mwujiza wo wote, lakini kila jambo alilosema kumhusu huyu mtu ni kweli.” 42Nao wengi wakamwamini Yesu huko.

Copyright information for Neno