John 12

Maria Ampaka Yesu Mafuta Huko Bethania

1Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alikwenda Bethania mahali ambako Lazaro aliyekuwa amefufuliwa na Yesu alikuwa anaishi. 2Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu. 3Kisha Maria akachukua chupa ya painti moja
12.3 Painti moja ni kama nusu lita
yenye manukato ya nardo
12.3 Nardo ni aina ya mafuta yaliyokuwa yanatengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri
safi ya thamani kubwa akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.

4Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wale wanafunzi ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema, 5“Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari 300
12.5 Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300
na fedha hizo wakapewa maskini?”
6Yuda alisema hivi si kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwivi, kwani ndiye aliyekuwa akitunza mfuko wa fedha akawa anaiba kile kilichowekwa humo.

7Yesu akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu. 8Maskini mnao siku zote lakini mimi hamko pamoja nami siku zote.”

Shauri La Kumwua Lazaro

9Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Yesu alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Yesu, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua. 10Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakafanya mpango wa kumwua Lazaro pia, 11kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake Wayahudi wengi walikuwa wanamwendea Yesu na kumwamini.

Kuingia Kwa Yesu Yerusalemu Kwa Ushindi

12Siku iliyofuata umati mkubwa uliokuwa umekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Yesu angekuja Yerusalemu. 13Basi wakachukua matawi ya mitende wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema, “Hosana
12:13 Kiebrania kusema Okoa, basi likawa neno la shangwe
!”
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”
“Amebarikiwa Mfalme wa Israeli!”14Yesu akamkuta mwana-punda akampanda, kama ilivyoandikwa, 15“Usiogope, Ewe binti Sayuni;
tazama, Mfalme wako anakuja,
amepanda mwana-punda!”16Wanafunzi wake Yesu mwanzoni hawakuelewa mambo haya, lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye.

17Wale waliokuwepo wakati Yesu alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu, waliendelea kushuhudia. 18Ni kwa sababu pia walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda mwujiza huu ndiyo maana umati wa watu ukaenda kumlaki. 19Hivyo Mafarisayo walipoona hayo wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lo lote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”

Yesu Anatabiri Kifo Chake

20Basi palikuwapo Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wamekwenda kuabudu wakati wa Sikukuu. 21Hawa wakamjia Filipo, ambaye alikuwa mwenyeji wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi, wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.” 22Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu.

23Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa. 24Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi. 25Mtu ye yote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata uzima wa milele. 26Mtu ye yote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.

27“Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe na saa hii.’ Lakini, ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu. 28Baba, litukuze jina lako.”

Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.”
29Ule umati wa watu uliokuwa mahali pale uliisikia nao ukasema, “Hiyo ni sauti ya radi,” wengine wakasema, “Malaika ameongea naye.”

30Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu. 31Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. 32Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka katika nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.” 33Yesu aliyasema haya akionyesha ni kifo gani atakachokufa.

34Ule umati wa watu ukapiga kelele ukasema, “Tumesikia kutoka katika Torati kwamba ‘Kristo
12:34 Yaani Masiya
adumu milele,’ wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu?’ Huyu ‘Mwana wa Adamu ni nani?’ ”

35Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingalipo pamoja nanyi. Enendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakokwenda. 36Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone.

Wayahudi Waendelea Kutokuamini

37Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. 38Hii ilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema:

“Bwana, ni nani aliyesadiki ujumbe wetu
na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?”39Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine: 40

“Amewafanya vipofu
na kuifanya mioyo yao kuwa migumu,
ili wasiweze kuona kwa macho yao,
wala kuelewa kwa mioyo yao,
wasije wakageuka, nami nikawaponya.”41Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake.

42Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi. 43Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu.

Amwaminiye Yesu Hatabaki Gizani

44Yesu akapaza sauti akasema, “Ye yote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali yeye aliyenituma. 45Ye yote anionaye mimi, amemwona yeye aliyenituma. 46Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kwamba kila mtu aniaminiye asibaki gizani.

47“Mimi simhukumu mtu ye yote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. 48Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. 49Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. 50Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lo lote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”

Copyright information for Neno