John 18

Yesu Akamatwa

1Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani, yeye na wanafunzi wake wakaingia humo.

2Basi Yuda, yule aliyemsaliti alipafahamu mahali hapo kwani Yesu alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara. 3Hivyo Yuda akaja bustanini, akiongoza kikosi cha maaskari wa Kirumi na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo, wakiwa wamechukua taa, mienge na silaha.

4Yesu akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao akawauliza, “Mnamtafuta nani?”

5Wao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.”

Yesu akawajibu, “Mimi ndiye.” Yuda, yule aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao.
6Yesu alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini!

7Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?”

Nao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.”

8Yesu akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa, mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.” 9Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.”

10Simoni Petro aliyekuwa na upanga akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa Kuhani Mkuu. Jina la mtumishi huyo aliitwa Malko.

11Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?”

Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu

12Hivyo wale maaskari wakiwa pamoja na majemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Yesu na kumfunga. 13Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule. 14Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu.

Petro Anamkana Yesu

15Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walikuwa wakimfuata Yesu. Huyu mwanafunzi mwingine alikuwa anafahamika kwa Kuhani Mkuu, hivyo aliingia ndani ya ukumbi pamoja na Yesu. 16Lakini Petro alisimama nje karibu na lango, ndipo yule mwanafunzi mwingine akazungumza na msichana aliyekuwa analinda lango, akamruhusu Petro aingie ndani.

17Yule msichana akamwuliza Petro, “Je, wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?”

Petro akajibu, “Mimi sio.”

18Wale watumishi na maaskari walikuwa wamesimama wakiota moto wa makaa kwa sababu palikuwa na baridi, Petro naye alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.

Kuhani Mkuu Amhoji Yesu

19Wakati huo Kuhani Mkuu akawa anamwuliza Yesu kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake.

20Yesu akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni mahali ambapo Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lo lote kwa siri. 21Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale walionisikia yale niliyowambia. Wao wanajua niliyosema.”

22Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa maaskari aliyekuwa amesimama karibu naye, akampiga Yesu kofi usoni, kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu Kuhani Mkuu?”

23Yesu akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?” 24Ndipo Anasi akampeleka Yesu kwa Kuhani Mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa.

Petro Amkana Yesu Tena

25Wakati huo Simoni Petro alikuwa amesimama akiota moto. Baadhi ya wale waliokuwepo wakamwuliza, “Je, wewe si mmoja wa wanafunzi wake?”

Petro akakana, akasema, “Mimi sio.”

26Mmoja wa watumishi wa Kuhani Mkuu, ndugu yake yule mtu ambaye Petro alikuwa amemkata sikio, akamwuliza, “Je, mimi sikukuona kule bustanini ukiwa na Yesu?” 27Kwa mara nyingine tena Petro akakana, naye jogoo akawika wakati uo huo.

Yesu Apelekwa Kwa Pilato

28Ndipo Wayahudi wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala wa Kirumi
18.28 Jumba la mfalme la mtawala wa Kirumi lilikuwa linaitwa Praitorio
. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri, ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Wangehesabiwa kuwa najisi kama wangeingia nyumbani mwa mtu asiye Myahudi na wasingeruhusiwa kushiriki katika Sikukuu ya Pasaka.
29Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?”

30Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu tusingemleta kwako.”

31Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.”

Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu ye yote.”
32Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Yesu kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia.

33Kwa hiyo Pilato akaingia ndani akamwita Yesu, akamwuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

34Yesu akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe au uliambiwa na watu kunihusu mimi?”

35Pilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”

36Yesu akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”

37Pilato akamwuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni ili niishuhudie kweli. Mtu ye yote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”

38Pilato akamwuliza Yesu, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Yesu, “Sioni kosa lo lote alilotenda mtu huyu. 39Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi?’ ”

40Wao wakapiga kelele wakisema, “Si huyu mtu bali tufungulie Baraba!” Basi Baraba alikuwa mnyang'anyi.

Copyright information for Neno