John 5

Yesu Amponya Mtu Penye Bwawa La Bethzatha

1Baada ya haya, kulikuwa na Sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. 2Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa kwa Kiebrania Bethzatha
5.2 Bethzatha ni neno la Kiebrania ambalo maana yake ni Nyumba ya mizeituni; mahali pengine limetajwa kama Bethesda kwa Kiaramu, yaani Nyumba ya huruma, na pengine kama Bethsaida, yaani Nyumba ya uvuvi
, ambalo lilikuwa limezungukwa na kumbi tano.
3Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani, vipofu, viwete, na waliopooza, wakingojea maji yatibuliwe 4[kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji na yule aliyekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wo wote aliokuwa nao]. 5Mtu mmoja alikuwako huko ambaye alikuwa ameugua kwa miaka thelathini na minane. 6Yesu alipomwona akiwa amelala hapo, naye akijua kuwa amekuwako hapo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?”

7Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.”

8Yesu akamwambia, “Simama, chukua mkeka wako na uende.” 9Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea.

Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato.
10Kwa hiyo Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, ni kinyume cha sheria wewe kubeba mkeka wako.”

11Yeye akawajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Chukua mkeka wako na uende.’ ”

12Wakamwuliza, “Ni mtu gani huyo aliyekuambia uchukue mkeka wako uende?”

13Basi yule mtu aliyeponywa hakufahamu ni nani aliyemponya, kwa sababu Yesu alikuwa amejiondoa katika ule umati wa watu uliokuwa hapo.

14Baadaye Yesu akamkuta yule mtu aliyemponya ndani ya Hekalu na kumwambia, “Tazama umeponywa, usitende dhambi tena. La sivyo, lisije likakupata jambo baya zaidi.” 15Yule mtu akaenda, akawaambia wale Wayahudi kuwa ni Yesu aliyemponya.

Uzima Kupitia Mwana

16Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumsumbua, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato. 17Yesu akawajibu, “Baba yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.” 18Maneno haya yaliwaudhi sana viongozi wa Wayahudi. Wakajaribu kila njia wapate jinsi ya kumwua, kwani si kwamba alivunja Sabato tu, bali alikuwa akimwita Mungu Baba yake, hivyo kujifanya sawa na Mungu.

Mamlaka Ya Mwana Wa Mungu

19Yesu akawaambia, “Amin, amin, nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lo lote peke yake, yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lo lote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo. 20Baba ampenda Mwana na kumwonyesha yale ambayo yeye Baba mwenyewe anayafanya, naye atamwonyesha kazi kuu kuliko hizi ili mpate kushangaa. 21Hakika kama vile Baba awafufuavyo wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo Mwana huwapa uzima wale anaopenda. 22Wala Baba hamhukumu mtu ye yote, lakini hukumu yote amempa Mwana, 23ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Ye yote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma.

24“Amin, amin ninawaambia, ye yote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani. 25Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia watakuwa hai. 26Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake. 27Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu.

28“Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake. 29Nao watatoka nje, wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima na wale waliotenda maovu, watafufuka wahukumiwe.

Shuhuda Kuhusu Yesu

30“Mimi siwezi kufanya jambo lo lote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.

31“Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. 32Lakini yuko mwingine anishuhudiaye na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli.

33“Mlituma wajumbe kwa Yohana, naye akashuhudia juu ya kweli. 34Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu, la, bali ninalitaja hili kusudi ninyi mpate kuokolewa. 35Yohana alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake.

36“Lakini ninao ushuhuda mkuu zaidi kuliko wa Yohana. Kazi zile nizifanyazo, zinashuhudia juu yangu, zile ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, ishara hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba ndiye aliyenituma. 37Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake, 38wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye. 39Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele, maandiko haya ndiyo yanayonishuhudia Mimi. 40Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima.

41“Mimi sitafuti kutukuzwa na wanadamu. 42Lakini ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu. 43Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei, lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea. 44Ninyi mwawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamna bidii kupata utukufu utokao kwa Mungu?

45“Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba, mshtaki wenu ni Mose, ambaye mmemwekea tumaini lenu. 46Kama mngelimwamini Mose, mngeliniamini na mimi kwa maana aliandika habari zangu. 47Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Mose, mtaaminije ninayoyasema?”

Copyright information for Neno