John 6

Yesu Alisha Watu 5,000

Baada ya haya, Yesu alikwenda ng'ambo ya Bahari ya Galilaya, ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia. Umati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa. Kisha Yesu akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

Yesu alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.

Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili
6.7 Dinari 200 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 200; mshahara wa kibarua ulikuwa dinari moja kwa siku
, hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa kila mtu apate kidogo.”

Mmoja wa wanafunzi wake, aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati wote huu?”

10 Yesu akasema, “waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi, palikuwa na wanaume 5,000. 11 Ndipo Yesu akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wamekaa kwa kiasi walichohitaji. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.

12 Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee cho chote.” 13 Hivyo wakavikusanya wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vilivyobaki vya ile mikate mitano na samaki wale wawili wadogo.

14 Baada ya watu kuona mwujiza ule Yesu aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!” 15 Yesu akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.

Yesu Atembea Juu Ya Maji

16 Ilipofika jioni, wanafunzi wake walitelemka kwenda baharini. 17 Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu. Wakati huu kulikuwa tayari giza na Yesu alikuwa hajajumuika nao. 18 Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne
6.19 Maili tatu au nne ni kama kilomita 5 au 6
, walimwona Yesu akitembea juu ya maji akikaribia mashua, wakaogopa sana.
20 Lakini Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope.” 21 Ndipo kwa furaha wakamkaribisha kwenye mashua, na mara wakafika walikokuwa wanakwenda.

Watu Wanamtafuta Yesu

22 Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ng'ambo ya pili waliona kwamba palikuwepo na mashua moja tu na kwamba Yesu hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao. 23 Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Yesu kumshukuru Mungu. 24 Mara wale watu wakatambua kwamba Yesu hakuwepo hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Yesu.

Yesu Ni Mkate Wa Uzima

25 Walipomkuta Yesu ng'ambo ya bahari wakamwuliza, “Rabi, umefika lini huku?”

26 Yesu akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27 Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba amemtia muhuri.”

28 Ndipo wakamwuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”

29 Yesu akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”

30 Hivyo wakamwuliza, “Utafanya ishara gani ya mwujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani? 31 Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”

32 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Mose aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”

34 Wakamwambia, “Bwana, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”

35 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. 36 Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. 37 Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na ye yote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe. 38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni si ili kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake yeye aliyenituma. 39 Haya ndiyo mapenzi yake yeye aliyenituma, kwamba, nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali niwafufue siku ya mwisho. 40 Kwa maana mapenzi ya Baba yangu ni kwamba kila mmoja amtazamaye, Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele, nami nitawafufua siku ya mwisho.”

41 Wayahudi wakaanza kunung'unika kwa kuwa alisema, “Mimi ndimi mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu si Yesu, mwana wa Yosefu, ambaye baba yake na mama yake tunawajua? Anawezaje basi sasa kusema, ‘Nimeshuka kutoka mbinguni’?”

43 Hivyo Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unikiana ninyi kwa ninyi. 44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu kama asipovutwa na Baba aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. 45 Imeandikwa katika manabii, ‘Wote watafundishwa na Mungu.’ Ye yote amsikilizaye Baba na kujifunza kutoka kwake, huyo huja kwangu. 46 Hakuna mtu ye yote aliyemwona Baba isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu, yeye ndiye peke yake aliyemwona Baba. 47 Amin, amin nawambia, yeye anayeamini anao uzima wa milele. 48 Mimi ni mkate wa uzima. 49 Baba zenu walikula mana jangwani, lakini wakafa. 50 Lakini hapa kuna mkate utokao mbinguni, ambao mtu ye yote akiula, hatakufa. 51 Mimi ni mkate wa uzima ule uliotoka mbinguni. Mtu ye yote akiula mkate huu, ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu, ambao nitautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.”

52 Ndipo Wayahudi wakaanza kuhojiana vikali wao kwa wao wakisema, “Mtu huyu awezaje kutupatia mwili wake tuule?”

53 Hivyo Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54 Mtu ye yote aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele. Nami nitamfufua siku ya mwisho. 55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 Ye yote alaye mwili wangu na kunywa damu yangu, atakaa ndani yangu nami nitakaa ndani yake. 57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, na kama nami ninavyoishi kwa sababu ya Baba, hivyo anilaye mimi ataishi kwa sababu yangu. 58 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, si kama ule mkate baba zenu waliokula nao wakafa. Lakini yeye aulaye mkate huu ataishi milele.” 59 Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu.

Wafuasi Wengi Wamwacha Yesu

60 Wengi wa wafuasi wake waliposikia jambo hili wakasema, “Mafundisho haya ni magumu. Ni nani awezaye kuyapokea?”

61 Yesu alipojua kwamba wafuasi wake wananung'unika kuhusu mafundisho yake, akawaambia, “Je, jambo hili limewaudhi? 62 Ingekuwaje basi kama mngemwona Mwana wa Adamu akipaa kwenda zake huko alipokuwa kwanza? 63 Roho ndiye atiaye uzima, mwili haufai kitu. Maneno haya niliyowaambia ni Roho tena ni uzima. 64 Lakini baadhi yenu hamwamini.” Kwa maana Yesu alifahamu tangu mwanzo wale ambao hawangemwamini miongoni mwao na yule ambaye angemsaliti. 65 Akaendelea kusema, “Hii ndiyo sababu niliwaambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.”

66 Tangu wakati huo wafuasi wake wengi wakarejea nyuma wakaacha kumfuata.

67 Hivyo Yesu akawauliza wale wanafunzi wake kumi na wawili, “Je, ninyi pia mnataka kuondoka?”

68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tuondoke twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 69 Tunaamini na kujua kuwa wewe ndiwe Kristo Mwana wa Mungu aliye hai.”

70 Ndipo Yesu akajibu, “Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Lakini mmoja wenu ni ibilisi.” 71 (Hapa alikuwa anasema juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili, ndiye ambaye baadaye angemsaliti Yesu.)

Copyright information for Neno