John 9

Yesu Amponya Mtu Aliyezaliwa Kipofu

Yesu alipokuwa akipita, akamwona mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza, “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni huyu mtu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”

Yesu akawajibu, “Huyu mtu wala wazazi wake hawakutenda dhambi. Alizaliwa kipofu ili kazi za Mungu zidhihirishwe katika maisha yake. Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi. Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

Baada ya kusema haya, akatema mate ardhini, akatengeneza tope kwa mate na kumpaka yule mtu kipofu machoni. Kisha akamwambia, “Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.” (Siloamu, maana yake ni aliyetumwa.) Ndipo yule kipofu akaenda, akanawa, naye akarudi akiwa anaona.

Majirani zake na wale wote waliokuwa wamemwona hapo awali akiombaomba wakaanza kuuliza, “Je, huyu si yule aliyekuwa akiketi akiombaomba?” Wengine wakasema, “Ndiye.”

Wengine wakasema, “Siye, bali wamefanana.”

Lakini yeye akawaambia, “Mimi ndiye.”

10 Wakamwuliza, “Basi macho yako yalifumbuliwaje?”

11 Yeye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alitengeneza tope, akanipaka machoni mwangu, naye akaniambia nenda ukanawe katika Bwawa la Siloamu, ndipo nikanawa nami nikapata kuona!”

12 Wale wakamwuliza, “Yeye huyo mtu yuko wapi?”

Akawajibu, “Sijui.”

Mafarisayo Wachunguza Kuponywa Kwa Kipofu

13 Wakamleta kwa Mafarisayo yule mtu aliyekuwa kipofu hapo awali. 14 Basi siku hiyo Yesu alipotengeneza tope na kuyafungua macho ya huyo mtu ilikuwa Sabato. 15 Mafarisayo nao wakaanza kumwuliza alivyopata kuponywa. Naye akawaambia, “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nikanawa na sasa ninaona.”

16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Huyu mtu hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.”

Lakini wengine wakasema, “Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya miujiza kama hii?” Wakagawanyika.

17 Hivyo wakamwambia tena yule mtu aliyekuwa kipofu, “Wewe ndiwe uliyefumbuliwa macho, wasemaje kuhusu mtu huyo?” Maana macho yako ndiyo yaliyofumbuliwa.

Yeye akawajibu, “Yeye ni nabii.”

18 Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu, akapata kuona, mpaka walipowaita wazazi wake. 19 Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?”

20 Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu. 21 Lakini sisi hatujui ni kwa jinsi gani kwamba sasa anaona, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Mwulizeni, yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.” 22 Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa Wayahudi kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu ye yote atakayemkiri Yesu kuwa ndiye Kristo
9:22 Yaani Masiya
atafukuzwa kutoka katika sinagogi.
23 Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Mwulizeni.”

24 Hivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.”

25 Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.”

26 Wakamwuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?”

27 Akawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?”

28 Ndipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake, Sisi ni wanafunzi wa Mose. 29 Tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini kwa habari ya mtu huyu hatujui atokako.”

30 Yule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu! 31 Tunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii. 32 Tangu kuumbwa kwa ulimwengu hatujasikia kwamba mtu amemponya ye yote aliyekuwa kipofu. 33 Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lo lote.”

34 Wao wakamjibu, “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, nawe unajaribu kutufundisha?” Wakamfukuza atoke nje.

Upofu Wa Kiroho

35 Yesu aliposikia kuwa wamemfukuzia nje yule mtu aliyemfumbua macho, alimkuta akamwuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?”

36 Yule mtu akamjibu, “Yeye ni nani ili nipate kumwamini, niambie ili nipate kumwamini.”

37 Yesu akamjibu, “Umekwisha kumwona, naye anayezungumza nawe, ndiye.”

38 Yule mtu akasema, “Bwana, naamini.” Naye akamwabudu.

39 Yesu akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona, wawe vipofu.”

40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?”

41 Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.

Copyright information for Neno