John 13

Yesu Awanawisha Wanafunzi Wake Miguu

1Ilikuwa mara tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni, naam, aliwapenda hadi kipimo cha mwisho.

2Wakati alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu. 3Yesu akijua ya kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. 5Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.

6Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?”

7Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.”

8Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.”

Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.”

9Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, bali pamoja na mikono na kichwa pia!”

10Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.” 11Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi.

12Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala anayetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.

18“Sisemi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni ili maandiko yapate kutimia, ‘Yeye aliyekula chakula changu, ameinua kisigino chake dhidi yangu.’

19“Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye. 20Amin, amin, nawaambia, ye yote anayempokea yule niliyemtuma, anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.”

Yesu Anatabiri Kusalitiwa Kwake

21Baada ya kusema haya, Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. 23Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Yesu alimpenda sana alikuwa ameegama kifuani mwa Yesu. 24Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi akamwambia, “Mwulize anamaanisha ni nani.”

25Yule mwanafunzi akiwa amemwegemea Yesu akamwuliza, “Bwana tuambie ni nani?”

26Yesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. 27Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia.

Yesu akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda litende haraka.”
28Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa ameketi nao chakulani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia hivyo. 29Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Yesu alikuwa amemwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini cho chote. 30Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.

Yesu Atabiri Petro Kumkana

31Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe naye atamtukuza mara.

33“Watoto wangu, mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo. Mtanitafuta na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, vivyo hivyo sasa nawaambia na ninyi. Niendako, ninyi hamwezi kuja.

34“Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. 35Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu”

36Simoni Petro akamwuliza, “Bwana, unakwenda wapi?”

Yesu akamjibu, “Ninakokwenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.”

37Petro akamwuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako.”

38Yesu akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin nakuambia, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

Copyright information for Neno