John 16

1“Nimewaambia mambo haya yote ili msije mkaiacha imani. 2Watawatenga na masinagogi. Naam, saa yaja ambayo mtu ye yote atakayewaua atadhani kwa kufanya hivyo anamtumikia Mungu. 3Nao watawatenda haya kwa sababu hawamjui Baba wala mimi. 4Lakini nimewaambia ninyi mambo haya, ili saa hiyo ikiwadia mpate kukumbuka ya kuwa nilikuwa nimewaambia. Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.

Kazi Ya Roho Mtakatifu

5“Sasa mimi ninakwenda kwake yeye aliyenituma, lakini hakuna hata aniulizaye, ‘Unakwenda wapi?’ 6Kwa sababu nimewaambia mambo haya, mioyo yenu imejawa na huzuni. 7Lakini amin nawaambia, yafaa mimi niondoke kwa kuwa nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu, lakini nikienda nitamtuma kwenu. 8Naye atakapokuja, atauthibitishia ulimwengu kuhusu dhambi, haki na hukumu. 9Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi, 10kwa habari ya haki, kwa sababu ninakwenda kwa Baba, nanyi hamtaniona tena, 11kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.

12“Bado ninayo mambo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili sasa. 13Atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza awatie katika kweli yote. Yeye hatanena kwa ajili yake mwenyewe, bali atanena yale yote atakayosikia, naye atawaonyesha mambo yajayo. 14Atanitukuza mimi, kwa maana atayachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi. 15Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu. Ndiyo maana nimesema Roho atachukua yaliyo yangu na kuwajulisha ninyi.

16“Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona.”

Huzuni Itageuka Kuwa Furaha

17Baadhi ya wanafunzi wakaulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?’ Naye ana maana gani asemapo, ‘Kwa sababu ninakwenda kwa Baba?’ ” 18Wakaendelea kuulizana, “Ana maana gani asemapo, ‘Kitambo kidogo?’ Hatuelewi hilo analosema.”

19Yesu akatambua kuwa walitaka kumwuliza juu ya hilo, hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana nina maana gani niliposema, ‘Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona?’ 20Amin, amin nawaambia, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi. Ninyi mtahuzunika, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21Mwanamke anapokuwa na utungu wa kuzaa huwa na maumivu kwa sababu saa yake imewadia. Lakini mtoto akiisha kuzaliwa, yule mwanamke husahau maumivu hayo kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtoto ulimwenguni. 22Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi na furaha yenu hakuna awaondoleaye. 23Katika siku hiyo hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin nawaambia, kama mkimwomba Baba jambo lo lote kwa Jina langu, yeye atawapa. 24Mpaka sasa hamjaomba jambo lo lote kwa Jina langu. Ombeni nanyi mtapewa, ili furaha yenu ipate kuwa kamili.

Amani Kwa Wanafunzi

25“Nimewaambia mambo haya kwa mafumbo. Saa yaja ambapo sitazungumza nanyi tena kwa mafumbo bali nitawaeleza waziwazi kuhusu Baba. 26Siku hiyo mtaomba kwa Jina langu. Wala sitawaambia kwamba nitamwomba Baba kwa ajili yenu, 27kwa maana Baba mwenyewe anawapenda, kwa sababu mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28Nilitoka kwa Baba na kuja ulimwenguni, sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”

29Ndipo wanafunzi wake wakasema, “Sasa unazungumza waziwazi, wala si kwa mafumbo. 30Sasa tumejua kwamba wewe unajua mambo yote, wala hakuna haja ya mtu kukuuliza maswali. Kwa jambo hili tunaamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”

31Yesu akawajibu, “Je, sasa mnaamini? 32Saa inakuja, naam, imekwisha kuwadia, mtakapotawanyika kila mmoja kwenda nyumbani kwake na kuniacha peke yangu. Lakini mimi si peke yangu kwa sababu Baba yu pamoja nami. 33Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

Copyright information for Neno