John 21

Yesu Awatokea Wanafunzi Saba

1Baada ya haya Yesu akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia
21:1 Yaani Bahari ya Galilaya
. Yeye alijionyesha kwao hivi:
2Simoni Petro, Tomasi aitwaye Didimasi, yaani Pacha, Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja. 3Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi nakwenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutakwenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata cho chote.

4Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu.

5Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wo wote?”

Wakamjibu, “La.”

6Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.

7Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia haya, akajifunga nguo yake kwa kuwa alikuwa uchi, naye akajitosa baharini. 8Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200
21.8 Dhiraa 200 ni kama mita 90
.
9Walipofika pwani, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate.

10Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”

11Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika. 12Yesu akawaambia, “Njoni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza, “Wewe ni nani?” Kwa sababu walijua ya kuwa ni Bwana. 13Yesu akaja, akachukua ule mkate, akawapa na vivyo hivyo akawagawia pia wale samaki. 14Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake tangu afufuke kutoka kwa wafu.

Yesu Amwuliza Petro Kama Anampenda

15Walipokwisha kula, Yesu akamwuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”

Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”

16Yesu akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”

Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Chunga kondoo zangu.”

17Kwa mara ya tatu Yesu akamwuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”

Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimwuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”

Yesu akamwambia, “Lisha kondoo zangu.
18Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka, lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.” 19Yesu alisema haya ili kuashiria ni kifo cha aina gani Petro atakachomtukuza nacho Mungu. Kisha Yesu akamwambia Petro, “Nifuate!”

20Petro akageuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Yesu walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”) 21Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamwuliza Yesu, “Bwana na huyu je?”

22Yesu akamjibu, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!” 23Kwa sababu ya maneno haya ya Yesu, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini?”

24Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya na ndiye ambaye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.

25Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Yesu alifanya. Kama yote yangeliandikwa, nadhani hata ulimwengu wote usingekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu vyote ambavyo vingeandikwa. Amen.

Copyright information for Neno