Joshua 11

Wafalme Wa Kaskazini Washindwa

Ikawa Yabini mfalme wa Hazori aliposikia habari za mambo haya, akatuma ujumbe kwa Yobabu mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na kwa mfalme wa Akshafu, na pia kwa wafalme wa upande wa kaskazini wale waliokuwa milimani, katika Araba upande wa kusini mwa Kinerethi, nchi chini ya vilima upande wa magharibi na katika miinuko ya Nafoth-Dori upande wa magharibi; kwa Wakanaani upande wa mashariki na magharibi; kwa Waamori, Wahiti, Waperizi na Wayebusi katika nchi ya vilima; na kwa Wahivi chini ya Hermoni katika nchi ya Mispa. Wakaja na vikosi vyao vyote na hesabu kubwa ya magari ya kuvutwa na farasi, jeshi kubwa, kama wingi wa mchanga ulio pwani ya bahari. Wafalme hao wote wakaunganisha majeshi yao na kupiga kambi pamoja penye Maji ya Meromu, ili kupigana dhidi ya Israeli.

BWANA akamwambia Yoshua, “Usiwaogope, kwa sababu kesho saa kama hii nitawatia wote mikononi mwa Israeli, wakiwa wameuawa. Utakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuyachoma moto magari yao.”

Hivyo Yoshua pamoja na jeshi lake lote wakaja dhidi yao ghafula na kwenye maji ya Meromu kuwashambulia, naye BWANA akawatia mikononi mwa Israeli. Wakawashinda na kuwafukuza hadi Sidoni Kuu na kuwafikisha Misrefoth-Maimu, hadi Bonde la Mispa upande wa mashariki, hadi pakawa hakuna ye yote aliyebaki. Yoshua akawatendea kama BWANA alivyomwamuru. Akakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuchoma moto magari yao.

10 Wakati huo Yoshua akarudi kuuteka mji wa Hazori na kumwua mfalme wake kwa upanga. (Hazori ulikuwa mji mkuu wa falme hizo zote.) 11 Kila aliyekuwa ndani yake wakamwua kwa upanga. Wakawaangamiza kabisa, wala hawakusaza cho chote chenye pumzi na akauchoma Hazori kwa moto.

12 Yoshua akaiteka hii miji yote ya kifalme pamoja na wafalme wake na kuwapiga kwa upanga. Akawaangamiza kabisa wote, kama Mose mtumishi wa BWANA alivyowaagiza. 13 Lakini Israeli hawakuichoma moto hata mojawapo ya miji hiyo iliyojengwa katika vilima vya hao wafalme, isipokuwa mji wa Hazori ambao Yoshua aliuchoma moto. 14 Waisraeli wakajichukulia nyara zote na mifugo yote ya miji hii, bali waliwaua watu wote kwa upanga hadi walipowaangamiza kabisa, wala hawakumbakiza ye yote mwenye pumzi. 15 Kama vile BWANA alivyomwagiza Mose mtumishi wake, vivyo hivyo Mose alimwagiza Yoshua, naye Yoshua akafanya kama vile alivyoagizwa, akafanya yote kwa uangalifu kama vile BWANA alivyomwagiza Mose.

16 Yoshua akaiteka nchi hii yote: nchi ya vilima, Negebu yote, nchi yote ya Gosheni, nchi chini ya vilima upande wa magharibi, Araba na milima ya Israeli pamoja na nchi chini ya vilima, 17 kuanzia Mlima Halaki ambao umeinuka kuelekea Seiri hadi Baal-Gadi katika Bonde la Lebanoni chini ya Mlima Hermoni. Akawateka wafalme wake wote akawapiga na kuwaua. 18 Yoshua akapigana vita dhidi ya wafalme hawa wote kwa muda mrefu. 19 Hakuna ye yote katika eneo hili aliyetafuta amani na Israeli, isipokuwa hao Wahivi wa Gibeoni. Wengine wote walishindwa. 20 Kwa maana ni BWANA mwenyewe ambaye aliifanya mioyo yao iwe migumu ili kupigana vita dhidi ya Israeli ili kwamba apate kuwafutilia mbali, pasipo huruma, kama BWANA alivyomwagiza Mose.

21 Wakati huo Yoshua akaenda kuwaangamiza Waanaki kutoka katika nchi ya vilima: kuanzia Hebroni, Debiri na Anabu, na kutoka katika nchi yote ya milima ya Yuda na kutoka katika nchi yote ya milima ya Israeli. Yoshua akawaangamiza kabisa pamoja na miji yao. 22 Hawakubaki Waanaki wo wote katika nchi ya Israeli, ila katika nchi ya Gaza, Gathi na Ashdodi. 23 Yoshua akaiteka nchi hiyo yote kama BWANA alivyokuwa amemwagiza Mose, naye Yoshua akawapa Israeli kuwa urithi wao, kama walivyogawanyika katika kabila zao.

Ndipo nchi ikawa na amani bila vita.

Copyright information for Neno