Joshua 16

Mgawo Kwa Ajili Ya Efraimu Na Manase

1Mgawanyo wa Yosefu ulianzia Yordani ya Yeriko, mashariki mwa miji ya Yeriko na kutoka hapo ulipanda kupitia jangwani na kuingia katika nchi ya vilima ya Betheli. 2Ukaendelea kutoka Betheli (ndiyo Luzu), ukavuka kuingia nchi ya Waariki huko Atarothi, 3ukatelemkia kuelekea magharibi hadi nchi ya Wayafleti mpaka sehemu ya Beth-Horoni ya Chini hadi Gezeri, ukiishia baharini.

4Kwa hiyo Manase na Efraimu, wazao wa Yosefu, walipokea urithi wao.5Hii ndiyo iliyokuwa nchi ya Efraimu, ukoo kwa ukoo:

Mpaka wa urithi wao ulianzia Atarothi Adari upande wa mashariki hadi Beth-Horoni ya Juu,
6na kuendelea mpaka baharini. Kutoka Mikmethathi upande wa kaskazini ulipinda kuelekea mashariki mpaka Taanath-Shilo, ukipitia Yanoa upande wa mashariki. 7Kisha ulitelemkia kutoka Yanoa hadi Atarothi na Naara, ukagusa Yeriko na kutokea katika Mto Yordani. 8Kutoka Tapua mpaka ulikwenda magharibi hadi Kijito cha Kana na kuishia baharini. Huu ulikuwa ndio urithi wa kabila la Waefraimu, ukoo kwa ukoo. 9Pia ulijumuisha miji yote na vijiji vyake ambavyo vilitengwa kwa ajili ya Waefraimu ndani ya urithi wa kabila la Manase.10Hawakuwafukuza Wakanaani waishio Gezeri; mpaka leo Wakanaani wanaishi miongoni mwa watu wa Efraimu lakini wanatakiwa kufanya kazi ngumu za kulazimishwa.

Copyright information for Neno