Joshua 18

Mgawanyo Wa Nchi Iliyobaki

Kusanyiko lote la Waisraeli likakusanyika huko Shilo na kusimamisha Hema ya Mkutano. Nchi ikawa chini ya utawala wao, lakini palikuwa bado makabila saba ya Israeli ambayo yalikuwa hayajapokea urithi wao.

Hivyo Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtasubiri hata lini ili kuingia kumiliki nchi ambayo BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa? Chagueni watu watatu kutoka kwenye kila kabila. Nitawatuma hao watu kukagua hiyo nchi ambayo bado haijatekwa, nao watanirudia wakiwa na taarifa ya mapendekezo ya mgawanyo wa urithi wa kila kabila. Mtaigawanya hiyo nchi sehemu saba. Yuda atabaki katika nchi yake upande wa kusini na nyumba ya Yosefu katika nchi yake upande wa kaskazini. Baada ya kuandika maelezo ya hizo sehemu saba za nchi, myalete kwangu, nami nitawagawia kwa kura mbele za BWANA Mungu wetu. Hata hivyo, Walawi hawatakuwa na sehemu miongoni mwenu, maana huduma ya ukuhani kwa BWANA ndio urithi wao. Nao Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase wameshapata urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, ambako Mose mtumishi wa BWANA aliwapa.”

Hivyo hao watu walipokuwa wanaondoka kwenda kuandika vizuri kuhusu hiyo nchi, Yoshua akawaagiza, “Nendeni mkakague hiyo nchi na mwandike maelezo yake. Kisha mrudi kwangu, nami nitawapigia kura hapa Shilo mbele za BWANA.” Ndipo hao watu walipoondoka na kupita katika ile nchi yote. Wakaandika maelezo yake, mji kwa mji, katika sehemu saba kwenye kitabu na kurudisha taarifa kwa Yoshua huko kambini Shilo. 10 Basi Yoshua akapiga kura kwa ajili yao huko Shilo mbele za BWANA, akagawanya nchi kwa Waisraeli kwa kufuatana na mgawanyo wa kabila zao.

Mgawo Kwa Benyamini

11 Kura iliangukia kabila la Benyamini, ukoo kwa ukoo. Nchi yao waliyogawiwa ilikuwa kati ya kabila la Yuda na la Yosefu.

12 Upande wa kaskazini mpaka wao ulianzia Yordani, kupitia kaskazini ya mtelemko wa Yeriko na kuendelea magharibi kuingia katika nchi ya vilima, ukitokea kwenye jangwa la Beth-Aveni. 13 Kutoka hapo ulikatiza kwenye mtelemko wa kusini wa Luzu (yaani Betheli) na kushuka hadi Ataroth-Adari katika kilima kusini mwa Beth-Horoni ya chini.

14 Kutoka kilima kinachotazamana na Beth-Horoni upande wa kusini mpaka ulizunguka kusini kufuatia upande wa magharibi, ukatokezea Kiriath-Baali (yaani Kiriath-Yearimu), mji wa watu wa Yuda. Huu ndio uliokuwa upande wa magharibi.

15 Upande wa kusini mpaka ulianzia kwenye viunga vya Kiriath-Yearimu kwa upande wa magharibi, nao ukatokeza kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa. 16 Mpaka ukatelemka hadi kwenye mwanzo wa mlima unaotazamana na Bonde la Ben-Hinomu, kaskazini ya Bonde la Warefai. Ukaendelea chini kwenye Bonde la Hinomu na kupitia mtelemko wa kusini wa mji wa Wayebusi na kisha hadi En-Rogeli. 17 Kisha ukapinda kuelekea kaskazini, ukaenda hadi En-Shemeshi na kuendelea mpaka Gelilothi, inayotazamana na Njia ya Adumimu, ukatelemka hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. 18 Ukaendelea upande wa mtelemko wa kaskazini wa Beth-Araba ukatelemka hadi Araba. 19 Kisha ukaendelea mpaka kwenye mtelemko wa kaskazini wa Beth-Hogla na kujitokeza kwenye ghuba ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi, kwenye maingilio ya Mto Yordani upande wa kusini. Huo ndio uliokuwa mpaka wa kusini.

20 Mto Yordani ulikuwa ndio mpaka wa upande wa mashariki.

Hii ilikuwa ndiyo mipaka iliyoonyesha urithi wa koo za Benyamini pande zote.21 Kabila za Benyamini, ukoo kwa ukoo, zilikuwa na miji ifuatayo:

Yeriko, Beth-Hogla, Emeki-Kesisi,
22 Beth-Araba, Semaraimu, Betheli, 23 Avimu, Para na Ofra, 24 Kefar-Amoni, Ofni, na Geba; miji kumi na miwili pamoja na vijiji vyake.

25 Gibeoni, Rama na Beerothi, 26 Mispa, Kefira, Moza, 27 Rekemu, Irpeeli, Tarala, 28 Zela, Elefu, mji wa Wayebusi (yaani Yerusalemu), Gibea na Kiriathi; miji kumi na minne pamoja na vijiji vyake.

Huu ndio uliokuwa urithi wa Benyamini kwa ajili ya koo zake.

Copyright information for Neno