Joshua 3

Kuvuka Yordani

Yoshua na Waisraeli wote wakaondoka asubuhi na mapema kutoka Shitimu, wakaenda mpaka Mto Yordani, ambako alipiga kambi kabla ya kuvuka. Baada ya siku tatu maafisa wakapita katika kambi yote, wakitoa maagizo kwa watu, wakiwaambia: “Mtakapoona Sanduku la Agano la BWANA Mungu wenu, likichukuliwa na Walawi ambao ndio makuhani, mtaondoka hapo mlipo na kulifuata. Ndipo mtakapotambua njia mtakayoiendea, kwa kuwa hamjawahi kuipita kabla. Lakini msisogee karibu, bali kuwe na umbali wa dhiraa 2,000
3.4 Dhiraa 2,000 ni sawa na mita 600
kati yenu na Sanduku.”

Ndipo Yoshua akawaambia hao watu, “Jitakaseni, kwa kuwa kesho BWANA atatenda mambo ya kushangaza katikati yenu.”

Yoshua akawaambia makuhani, “Liinueni Sanduku la Agano mkatangulie mbele ya watu.” Hivyo wakaliinua na kutangulia mbele yao.

Ndipo BWANA akamwambia Yoshua, “Leo nitaanza kukutukuza machoni pa Israeli yote, ili wapate kujua kuwa niko pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. Uwaambie makuhani wanaochukua Sanduku la Agano, ‘Mnapofika kwenye ukingo wa maji ya Yordani, nendeni mkasimame ndani ya mto.’ ”

Yoshua akawaambia Waisraeli, “Njoni hapa msikilize maneno ya BWANA Mungu wenu. 10 Hivi ndivyo mtakavyojua yakuwa Mungu aliye hai yupo katikati yenu na kwamba kwa hakika atawafukuza mbele yenu hao Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi. 11 Tazama, Sanduku la Agano la BWANA wa dunia yote litaingia ndani ya Mto Yordani likiwa limetangulia. 12 Sasa basi, chagueni watu kumi na wawili kutoka katika makabila ya Israeli, mtu mmoja kutoka kila kabila. 13 Mara tu nyayo za makuhani walichukualo Sanduku la BWANA, Bwana wa dunia yote, zitakapokanyaga ndani ya Mto Yordani, maji hayo yatiririkayo kutoka juu yatatindika na kusimama kama chuguu.”

14 Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia. 15 Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji, 16 maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yalitindika yakasimama kama chuguu mbali nao, kwenye mji ulioitwa Adamu karibu na Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalikauka kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.

17 Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la BWANA, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lile lote likaisha kuvuka mahali pakavu.

Copyright information for Neno