Joshua 5

1Basi wafalme wote wa Waamori magharibi ya Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye mwambao wa bahari waliposikia jinsi BWANA alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri kuwakabili Waisraeli.

Tohara Huko Gilgali

2Wakati huo BWANA akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya mawe magumu sana na uwatahiri Waisraeli.” 3Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya mawe magumu sana na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi
5.3 Gibeath-Haaralothi maana yake ni Kilima cha Magovi
.

4Hii ndiyo sababu ya kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani, baada ya kuondoka Misri. 5Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini toka Misri walikuwa hawajatahiriwa. 6Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini mpaka wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati walipoondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii BWANA. Kwa maana BWANA alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao kuwapatia, nchi inayotiririka maziwa na asali. 7Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini. 8Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini mpaka walipokuwa wamepona.

9BWANA akamwambia Yoshua, “Leo nimeiondoa aibu ya Wamisri kutoka kwenu.” Basi mahali pale pakaitwa Gilgali hadi leo.

10Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa kambini huko Gilgali katika tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka. 11Siku ya pili baada ya Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi, mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga. 12Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani.

Amiri Jeshi Wa Jeshi La BWANA

13Basi wakati Yoshua alipokaribia Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi uliofutwa kwenye ala. Yoshua akamwendea na kumwuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?”

14Akajibu, “La, siko upande wo wote, lakini mimi nimekujia nikiwa amiri jeshi wa jeshi la BWANA.” Yoshua akaanguka kifudifudi hadi nchi, akasujudu, akamwuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?” 15Amiri jeshi wa jeshi la BWANA akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.

Copyright information for Neno