Joshua 22

Makabila Ya Mashariki Yarudi Nyumbani

1Ndipo Yoshua akawaita Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, 2naye akawaambia, “Mmeshafanya yale yote Mose mtumishi wa BWANA aliyowaamuru, nanyi mmenitii kwa kila jambo nililowaamuru. 3Kwa muda mrefu sasa, hadi siku hii ya leo, hamkuwaacha ndugu zenu, bali ninyi mmetimiza ile kazi BWANA Mungu wenu aliyowapa. 4Sasa kwa kuwa BWANA Mungu wenu amewapa ndugu zenu raha kama alivyoahidi, rudini nyumbani mwenu katika nchi ile ambayo Mose mtumishi wa BWANA aliwapa ng'ambo ya pili ya Yordani. 5Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria zile Mose mtumishi wa BWANA alizowapa: yaani kumpenda BWANA Mungu wenu na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wenu wote na roho yenu yote.”

6Ndipo Yoshua akawabariki na kuwaaga waende zao, nao wakaenda nyumbani mwao. 7(Kwa nusu ya kabila la Manase Mose alikuwa amewapa eneo katika Bashani na ile nusu nyingine Yoshua aliwapa eneo upande wa magharibi ya Yordani pamoja na ndugu zao.) Yoshua alipowapeleka waende zao nyumbani mwao, aliwabariki, 8akisema, “Rudini ninyi nyumbani mwenu na utajiri wenu, yaani makundi makubwa ya mifugo, mkiwa na fedha, dhahabu, shaba na chuma, pia wingi wa nguo, nanyi mkagawane na ndugu zenu hizo nyara zilizotoka kwa adui zenu.”

9Kwa hiyo Wareubeni, Wagadi na hiyo nusu ya kabila la Manase wakawaacha Waisraeli huko Shilo katika nchi ya Kanaani ili kurudi Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoipata sawasawa na agizo la BWANA kupitia Mose.

10Walipofika Gelilothi karibu na Yordani, katika nchi ya Kanaani, Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakajenga madhabahu ya fahari kubwa huko kando ya Yordani. 11Wale Waisraeli wengine waliposikia kwamba Wareubeni, Wagadi na ile nusu ya kabila la Manase walikuwa wamejenga madhabahu upande wa magharibi mwa Yordani kwenye mpaka wa Kanaani huko Gelilothi, 12kusanyiko lote la Israeli wakakusanyika huko Shilo ili wakapigane vita dhidi yao.

13Kwa hiyo hao Waisraeli wengine wakamtuma Finehasi mwana wa kuhani Eleazari katika nchi ya Gileadi, aende kwa Wareubeni, Wagadi na hiyo nusu ya kabila la Manase. 14Wakatuma pamoja naye watu kumi ambao ni viongozi, mmoja kwa ajili ya kila kabila la Israeli, kila mmoja aliye kiongozi katika mgawanyiko wa jamaa miongoni mwa koo za Israeli.

15Walipofika katika nchi ya Gileadi, kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, wakawaambia: 16“Kusanyiko lote la BWANA lasema: ‘Je, mmewezaje kuacha kumwamini Mungu wa Israeli kwa kufanya jambo kama hili? Mmewezaje kumwacha BWANA na sasa kujijengea madhabahu dhidi yake na kumwasi? 17Je, dhambi ya Peori ilikuwa ndogo sana kwetu? Mpaka leo hatujatakasika kutokana na dhambi hiyo, hata ingawa kulikuja tauni juu ya kusanyiko la BWANA! 18Je, sasa ndiyo mnamwacha BWANA?

“ ‘Kama mkimwasi BWANA leo, kesho atalikasirikia kusanyiko lote la Israeli.
19Kama nchi mnayomiliki imenajisika, vukeni mje katika nchi ya BWANA, mahali Maskani ya BWANA ilipo, nanyi mkajitwalie sehemu miongoni mwetu, lakini msije mkaasi dhidi ya BWANA wala dhidi yetu sisi kwa kujijengea madhabahu nyingine kwa ajili yenu, zaidi ya madhabahu ya BWANA Mungu wetu. 20Wakati Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu kwa vitu vilivyowekwa wakfu, je, ghadhabu ya Mungu haikulipata kusanyiko lote la Israeli? Wala hakuwa yeye peke yake aliyekufa kwa ajili ya hiyo dhambi yake.’ ”

21Ndipo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walipowajibu viongozi wa koo za Israeli, wakisema: 22“Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, BWANA! Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, BWANA! Yeye anajua! Israeli na wajue! Kama hili limekuwa ni kuasi au kukosa utii kwa BWANA, asituache hai siku hii ya leo. 23Kama tumejijengea madhabahu yetu wenyewe ili kumwacha BWANA na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, au kutoa sadaka za amani juu yake, BWANA mwenyewe na atupatilize leo.

24“Sivyo! Tulifanya hivyo kwa hofu kwamba siku zijazo wazao wenu wanaweza wakawaambia wazao wetu, ‘Mna uhusiano gani na BWANA, Mungu wa Israeli? 25BWANA ameifanya Yordani kuwa mpaka kati yetu na ninyi, ninyi Wareubeni na Wagadi! Hamna fungu kwa BWANA.’ Kwa hiyo wazao wenu wanaweza wakawasababisha wazao wetu wakaacha kumcha BWANA.

26“Hii ndiyo sababu tulisema, ‘Tujiweke tayari na tujenge madhabahu, lakini si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa au dhabihu.’ 27Badala yake, itakuwa ni ushahidi kati yetu na ninyi na vizazi vijavyo, kwamba tutamwabudu BWANA katika mahali patakatifu pake pamoja na sadaka zetu za kuteketezwa, dhabihu na sadaka za amani. Ndipo siku zijazo wazao wenu hawataweza kuwaambia wazao wetu, ‘Ninyi hamna fungu katika BWANA.’

28“Nasi tulisema, ‘Ikiwa wakati wo wote watatuambia hilo, au kuwaambia uzao wetu, tutawajibu hivi: Angalieni nakala hii ya madhabahu ya BWANA, ambayo baba zetu waliijenga, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu, bali kama ushahidi kati yetu sisi na ninyi.’

29“Hili jambo la kumwasi BWANA na kumwacha siku hii ya leo kwa kujenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na dhabihu, zaidi ya madhabahu ya BWANA Mungu wetu iliyo mbele ya maskani yake na liwe mbali nasi.”

30Wakati kuhani Finehasi na viongozi wa kusanyiko, wakuu wa koo za Israeli, waliposikia hayo waliyosema hao Wareubeni, Wagadi na hiyo nusu ya kabila la Manase, wakaridhika. 31Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akawaambia hao Wareubeni, Wagadi na hiyo nusu ya kabila la Manase, “Leo tunajua kwamba BWANA yuko pamoja nasi, kwa sababu hamkukosa uaminifu kwa BWANA katika jambo hili. Sasa mmewaokoa Waisraeli na mkono wa BWANA.”

32Ndipo Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari na viongozi wakarudi Kanaani kutoka kwenye kukutana kwao na Wareubeni na Wagadi huko Gileadi nao wakatoa taarifa kwa Waisraeli. 33Walifurahi kusikia taarifa hiyo, nao wakamhimidi Mungu. Wala hawakuzungumza tena habari za kupigana vita dhidi yao kuharibu nchi ambayo Wareubeni na Wagadi waliishi.

34Nao Wareubeni na Wagadi wakaiita ile madhabahu Edi, yaani Shahidi: kwa kuwa itakuwa shahidi kati yetu na ninyi kwamba BWANA ndiye Mungu.

Copyright information for Neno