Joshua 23

Yoshua Anawaaga Viongozi

1Baada ya muda mrefu kupita, naye BWANA alikuwa amewapa Israeli raha mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo alikuwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana, 2akawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa wao, na kuwaambia: “Mimi ni mzee na umri umeendelea sana. 3Ninyi wenyewe mmeona kila kitu BWANA Mungu wenu, alichowatendea makabila haya yote kwa ajili yenu, ilikuwa ni BWANA Mungu wenu aliyewapigania. 4Kumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa ajili ya makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari ile kuu upande wa magharibi. 5BWANA Mungu wenu mwenyewe, atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vile BWANA Mungu wenu alivyowaahidi.

6“Iweni hodari sana, iweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Torati ya Mose, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto. 7Msishirikiane na mataifa yaliyobakia katikati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia. 8Bali mtashikamana kwa uthabiti na Mungu wenu, kama vile ambavyo mmefanya mpaka sasa.

9“BWANA amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, mpaka siku ya leo hakuna ye yote aliyeweza kusimama mbele yenu. 10Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu, kwa kuwa BWANA Mungu wenu anawapigania, kama alivyoahidi. 11Kwa hiyo iweni waangalifu sana kumpenda BWANA Mungu wenu.

12“Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia katikati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao, 13basi mwe na hakika kuwa BWANA Mungu wenu hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu na miiba machoni penu, mpaka mwangamie kutoka katika nchi hii nzuri, ambayo BWANA Mungu wenu amewapa.

14“Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zo zote njema BWANA Mungu wenu alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia. 15Bali kama vile ambavyo kila ahadi njema ya BWANA Mungu wenu imekuwa kweli, vivyo hivyo BWANA ataleta maovu yote aliyosema, mpaka awe amewaangamiza kutoka katika nchi hii nzuri aliyowapa. 16Kama mkilivunja Agano la BWANA Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya BWANA itawaka dhidi yenu, nanyi mtaangamia mara kutoka katika nchi nzuri aliyowapa ninyi.”

Copyright information for Neno