Joshua 24

Agano Lafanywa Upya Huko Shekemu

1Ndipo Yoshua akaita pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maafisa wa Israeli, nao wakaja mbele za Mungu.

2Yoshua akawaambia watu wote, “Hili ndilo BWANA, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Hapo zamani baba zenu, pamoja na Tera baba yake Abrahamu na Nahori, waliishi ng'ambo ya Mto Eufrati nao waliiabudu miungu mingine. 3Lakini nilimwondoa baba yenu Abrahamu kutoka nchi hiyo ng'ambo ya Mto, nami nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani, nikampa wazao wengi. Nikampa Isaki, 4naye Isaki nikampa Yakobo na Esau. Esau nikampa nchi ya vilima ya Seiri, lakini Yakobo pamoja na wanawe wakashuka Misri.

5“ ‘Kisha nikawatuma Mose na Aroni, nami nikawapiga Wamisri kwa kile nilichokitenda huko, tena nikawatoa huko. 6Nilipowatoa baba zenu katika nchi ya Misri, mlifika kwenye bahari, nao Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka kwenye Bahari ya Shamu. 7Lakini wakamlilia BWANA wakitaka msaada, Mungu akaweka giza kati yenu na Wamisri, akaileta bahari juu yao ikawafunika. Ninyi mliona kwa macho yenu wenyewe kile nilichowatendea Wamisri. Kisha mliishi jangwani kwa muda mrefu.

8“ ‘Nikawaleta katika nchi ya Waamori ambao waliishi mashariki ya Yordani. Wakapigana nanyi, lakini nikawatia mikononi mwenu. Nikawaangamiza mbele yenu nanyi mkaimiliki nchi yao. 9Wakati Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipojiandaa kupigana dhidi ya Israeli, alimwita Balaamu mwana wa Beori apate kuwalaani. 10Lakini sikumkubali Balaamu, kwa hiyo aliwabariki tena na tena, nami niliwaokoa toka mkononi mwake.

11“ ‘Ndipo mlipovuka Yordani mkafika Yeriko. Raia wa Yeriko wakapigana nanyi, kama walivyofanya Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi, lakini niliwatia mikononi mwenu. 12Nikatuma manyigu mbele yenu, ambao pia waliwafukuza mbele yenu, hao wafalme wawili wa Waamori. Siyo upanga au upinde wenu wenyewe vilivyowapatia ushindi. 13Hivyo nikawapa ninyi nchi ambayo hamkuitaabikia na miji ambayo hamkuijenga, mkaishi ndani yake na kula mizabibu na mizeituni msiyoipanda.’

14“Sasa basi mcheni BWANA na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ng'ambo ya Mto Eufrati na huko Misri, nanyi mtumikieni BWANA. 15Lakini msipoona vyema kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo Eufrati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia BWANA.”

16Ndipo hao watu wakajibu, “Hili liwe mbali nasi la kumsahau BWANA na kuitumikia miungu mingine! 17Ilikuwa ni BWANA Mungu wetu mwenyewe aliyetutoa sisi na baba zetu akatupandisha kutoka Misri, kutoka nchi ile ya utumwa, na kutenda zile ishara kubwa mbele ya macho yetu. Ndiye aliyetulinda katika safari yetu yote na kutokana na mataifa yote ambayo tulipita katikati yao. 18BWANA akawafukuza mbele yetu mataifa yote pamoja na Waamori, walioishi katika nchi hii. Hivyo sisi nasi tutamtumikia BWANA, kwa kuwa yeye ndiye Mungu wetu.”

19Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia BWANA. Yeye ni Mungu Mtakatifu, ni Mungu mwenye wivu. Hatasamehe uasi wenu na dhambi zenu. 20Ikiwa mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, yeye atageuka na kuwaleteeni maafa na kuwaangamiza, baada ya kuwa mwema kwenu.”

21Lakini watu wakamwambia Yoshua, “Sivyo! Sisi tutamtumikia BWANA.”

22Ndipo Yoshua akawaambia, “Ninyi mmekuwa mashahidi juu yenu wenyewe kuwa mmechagua kumtumikia BWANA.”

Nao wakajibu, “Ndiyo, tu mashahidi.”

23Yoshua akawaambia, “Sasa basi, itupeni mbali hiyo miungu migeni iliyo katikati yenu, nanyi mtoleeni BWANA, Mungu wa Israeli, mioyo yenu.”

24Nao watu wakamwambia Yoshua, “Tutamtumikia BWANA Mungu wetu na kumtii yeye.”

25Siku ile Yoshua akafanya agano kwa ajili ya watu na hapo Shekemu ndipo alipowaandikia amri na sheria. 26Naye Yoshua akayaandika mambo haya katika Kitabu cha Sheria ya Mungu. Ndipo akalitwaa jiwe kubwa akalisimamisha huko, chini ya mwaloni huko karibu na mahali patakatifu pa BWANA.

27Akawaambia watu wote, “Angalieni! Jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu. Limesikia maneno yote BWANA aliyotuambia. Litakuwa shahidi juu yenu kama mtakuwa waongo kwa Mungu wenu.”

Kuzikwa Katika Nchi Ya Ahadi

28Basi Yoshua akawatuma watu kila mmoja aende katika urithi wake mwenyewe.

29Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. 30Nao wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Sera
24:30 Unajulikana pia kama Timnath-Heresi, ona Yos 19:50; Amu 2:9
katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima wa Gashi.

31Israeli wakamtumikia BWANA wakati wote wa kipindi cha Yoshua, na kipindi cha hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa na ambao waliona wenyewe kila kitu BWANA alichowatendea Israeli.

32Nayo ile mifupa ya Yosefu, ambayo Waisraeli waliipandisha kutoka huko Misri, wakaizika huko Shekemu kwenye eneo, ambalo Yakobo alilinunua kwa wana wa Hamori baba yake Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Eneo hili likawa ni urithi wa uzao wa Yosefu.

33Naye Eleazari mwana wa Aroni akafariki akazikwa huko Gibeathi, ambapo alikuwa amepewa mtoto wake Finehasi, kwenye nchi ya vilima ya Efraimu.

Copyright information for Neno