Judges 12

Yefta Na Efraimu

Watu wa Efraimu wakaita majeshi yao, wakavuka kwenda Zafoni, wakamwambia Yefta, “Kwa nini mmekwenda kupigana na Waamoni bila kutuita ili tuende pamoja nawe? Basi tutaichoma moto nyumba yako, pamoja nawe ukiwa ndani yake.”

Yefta akajibu, “Mimi na watu wangu tulikuwa na ugomvi mkubwa na Waamoni, hata ingawa niliwaita hamkuniokoa katika mkono wao. Nilipoona kuwa hamkunipa msaada nikauhatarisha uhai wangu na nikavuka kupigana na Waamoni. Naye BWANA akanipatia ushindi dhidi yao. Sasa kwa nini mnanijia leo ili kupigana nami?”

Ndipo Yefta akakusanya watu wa Gileadi pamoja na kupigana na Efraimu. Wagileadi wakawashinda Efraimu, kwa kuwa Waefraimu walisema, “Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka toka Efraimu na Manase.” Wagileadi wakaviteka vivuko vya Yordani dhidi ya hao Waefraimu, kisha ilikuwa ye yote yule aliyenusurika katika Efraimu aliposema, “Niache nivuke,” hao watu wa Gileadi walimwuliza, “Je wewe ni Mwefraimu?” Kama alijibu “Hapana,” walimwambia, “Sawa, sema ‘Shibolethi.’ ” Iwapo alitamka, “Sibolethi,” kwa sababu hakuweza kutamka hilo neno sawasawa, walimkamata na kumwua hapo kwenye vivuko vya Yordani. Waefraimu 42,000 waliuawa wakati huo.

Yefta akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa muda wa miaka sita. Basi Yefta akafa, akazikwa katika mmojawapo wa miji ya Gileadi.

Ibzani, Eloni Na Abdoni

Baada yake, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli. Alikuwa na wana thelathini na binti thelathini. Akawaoza binti zake kwa watu wengine nje ya ukoo wake, na kuwatwalia wanawe wanawake thelathini toka nje ya ukoo wake. Ibzani akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka saba. 10 Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.

11 Baada yake Eloni, Mzabuloni, akawa mwamuzi wa Israeli, naye akawaamua kwa muda wa miaka kumi. 12 Kisha Eloni akafa, akazikwa katika Aiyaloni, katika nchi ya Zabuloni.

13 Baada yake, Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akawa mwamuzi wa Israeli. 14 Naye akazaa wana arobaini na wana wa wanawe thelathini waliopanda punda sabini. Akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka minane. 15 Ndipo Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akafa, naye akazikwa huko Pirathoni katika Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.

Copyright information for Neno