Judges 14

Ndoa Ya Samsoni

Samsoni akatelemkia Timna, akamwona mwanamke wa Kifilisti. Alipopanda kutoka huko, akawaambia baba yake na mama yake, “Nimemwona mwanamke wa Kifilisti huko Timna; basi mnipatie ili awe mke wangu.”

Baba yake na mama yake wakamjibu, “Je, hakuna mwanamke miongoni mwa jamaa yako au miongoni mwa ndugu zako, hata ulazimike kwenda kujitwalia mwanamke kutoka kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa?”

Lakini Samsoni akamwambia baba yake, “Nipatieni huyo kwa maana ndiye aliyenipendeza.”
(Baba yake na mama yake hawakujua kuwa jambo hili limetoka kwa BWANA, kwani alikuwa akitafuta sababu ya kukabiliana na Wafilisti; kwa kuwa wakati huo walikuwa wakiwatawala Waisraeli.) Samsoni akatelemkia Timna pamoja na baba yake na mama yake. Walipofika kwenye mashamba ya mizabibu huko Timna, ghafula mwana simba akamjia akimngurumia. Roho wa BWANA akaja juu yake kwa nguvu, naye akampasua yule simba kwa mikono yake bila silaha yo yote kama vile mtu ampasuavyo mwana-mbuzi, wala hakumwambia baba yake wala mama yake aliyoyafanya. Basi akatelemka na kuongea na yule mwanamke, naye akampendeza Samsoni.

Baada ya muda aliporudi ili akamwoe, akatazama kando ili kuutazama mzoga wa yule simba, na tazama, kulikuwa na kundi la nyuki ndani ya ule mzoga wa simba na kulikuwa na asali; akachukua asali mkononi mwake akaendelea huku akila. Alipowafikia baba yake na mama yake, akawapa ile asali nao wakala. Lakini hakuwaambia kuwa alitwaa asali kutoka kwenye mzoga wa simba.

10 Basi baba yake akatelemka kumwona huyo mwanamke. Samsoni akafanya karamu huko, kama ilivyokuwa desturi ya vijana. 11 Watu walipomwona, wakaleta vijana wenzake thelathini ili kuwa pamoja naye.

12 Samsoni akawaambia, “Niwape kitendawili, mkiweza kunipa jibu katika muda wa siku hizi saba za karamu, nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini. 13 Lakini msipoweza kufumbua, ndipo ninyi mtanipa mavazi thelathini ya kitani na mavazi mengine mivao thelathini.”

Wakamwambia, “Tuambie hicho kitendawili, hebu na tukisikie.”

14 Akawaambia, “Ndani ya mlaji,
kulitoka kitu cha kuliwa,
ndani ya mwenye nguvu,
kulitoka kitu kitamu.”Kwa muda wa siku tatu hawakuweza kutoa jibu.

15 Siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, “Mbembeleze mumeo ili atueleze hicho kitendawili, la sivyo tutakuchoma moto wewe na wa nyumba ya baba yako. Je, mmetualika ili mpate kutunyang'anya kile tulicho nacho?”

16 Basi mke wa Samsoni akalia mbele yake na kumwambia, “Unanichukia! Hunipendi kabisa. Umewategea watu wangu kitendawili, lakini mimi hujaniambia jibu.”

Samsoni akamwambia, “Wala sijamweleza baba yangu wala mama yangu, kwa nini nikufumbulie?”
17 Mkewe akalia kwa muda wa zile siku zote saba za karamu. Hivyo siku ile ya saba Samsoni akamweleza, kwa kuwa aliendelea kumsisitiza sana. Naye akawaeleza watu wake kile kitendawili.

18 Siku ya saba kabla ya jua kutua, watu wa mji wakamwambia Samsoni, “Ni nini kitamu kama asali?
Ni nini chenye nguvu kama simba?”Samsoni akawaambia, “Kama hamkulima na mtamba wangu,
hamngeweza kufumbua
kitendawili changu.”19 Ndipo Roho wa BWANA akamjia Samsoni kwa nguvu. Akatelemka mpaka Ashkeloni, akawaua watu waume thelathini miongoni mwa watu wa mji, akatwaa mali zao na nguo zao, akawapa watu wale waliofumbua kile kitendawili. Akiwa na hasira, akakwea kurudi nyumbani kwa baba yake. 20 Lakini huyo mke wa Samsoni akakabidhiwa kwa rafiki yake Samsoni ambaye alikuwa rafiki yake msaidizi siku ya arusi.

Copyright information for Neno