Judges 21

Wabenyamini Watafutiwa Wake

1Wana wa Israeli walikuwa wameapa kwa kiapo kule Mispa: “Hapana mtu awaye yote atakayemwoza binti yake kwa Wabenyamini.”

2Watu wakaenda Betheli, wakaketi mbele za Mungu mpaka jioni, wakapaza sauti zao, wakalia sana. 3Wakasema, “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limewapata Waisraeli? Kwa nini kabila moja la Israeli limekosekana?”

4Kesho yake asubuhi na mapema watu wakajenga madhabahu na kuleta sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.

5Ndipo Waisraeli wakasema, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikufika katika mkutano kumkaribia BWANA?” Kwa kuwa walikuwa wameweka kiapo kikuu kuwa ye yote asiyefika mbele za BWANA huko Mispa, kwa hakika angeuawa.

6Basi Waisraeli wakaghairi kwa ajili ya ndugu zao Wabenyamini, wakasema, “Leo kabila moja limekatiliwa mbali na Israeli. 7Sasa tutawezaje kuwapa mabinti zetu wawe wake zao kwa hao waliobakia maadamu tumeapa kuwa hatutawapa binti zetu kuwa wake zao?” 8Ndipo wakasema, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikufika mbele za BWANA huko Mispa?” Wakagundua kuwa hakuna hata mmoja aliyetoka Yabeshi-Gileadi aliyefika kambini kwa ajili ya kusanyiko la mkutano. 9Walipohesabu waliona hakuna mtu ye yote wa Yabeshi-Gileadi aliyekuwapo.

10Ndipo mkutano wakatuma askari kumi na wawili, wakawaamuru kwenda Yabeshi-Gileadi na kuwaua wale wote waishio huko, walikuwepo wake na watoto. 11Wakasema, “Hilo ndilo mtakalofanya. Ueni kila mtu mume na mke ambaye si bikira.” 12Wakawakuta watu waishio Yabeshi-Gileadi wanawali mia nne ambao hawajakutana kimwili, nao wakawachukuwa kwenye kambi huko Shilo katika nchi ya Kanaani.

13Ndipo mkutano ukatuma ujumbe wa amani kwa Wabenyamini huko katika mwamba wa Rimoni. 14Basi Wabenyamini wakarudi nyumbani mwao, wakapewa wale wanawali wa Yabeshi-Gileadi waliowaponya. Lakini hawakuwatosha wanaume wote.

15Waisraeli wakasikitika kwa ajili ya Wabenyamini, kwa kuwa BWANA ameweka ufa katika makabila ya Israeli. 16Viongozi wa kusanyiko wakasema, “Kwa kuwa wanawake wa Wabenyamini wameangamizwa, tufanyeje ili kuwapatia wake wale wanaume waliosalia? 17Wale waliopona wa Wabenyamini ni lazima tuwapatie wake, ili wawe na warithi, ili kabila lo lote katika Israeli lisifutike. 18Hatuwezi kuwapa binti zetu kuwa wake, kwa kuwa sisi Waisraeli tumeapa kiapo hiki: ‘Alaaniwe mtu ye yote ampaye Mbenyamini mke.’ ” 19Ndipo waliposema, “Tazama iko sikukuu ya kila mwaka ya BWANA katika Shilo, kaskazini ya Betheli na mashariki mwa ile barabara itokayo Betheli kwenda Shekemu, nako ni kusini ya Lebona.”

20Hivyo wakawaelekeza Wabenyamini wakisema, “Nendeni mkajifiche kwenye mashamba ya mizabibu, 21nanyi mwangalie. Wasichana wa Shilo watakapojiunga kwenye kucheza, ninyi tokeni kwenye hayo mashamba ya mizabibu na kila mmoja akamate mwanamke mmoja toka miongoni mwa hao wasichana wa Shilo na mwende nao katika nchi ya Benyamini. 22Baba zao au ndugu zao waume watakapotulalamikia, tutawaambia, ‘Iweni wakarimu kwetu, nanyi mturuhusu tuwe nao kwa kuwa hatukuweza kumpatia kila mtu mke tulipopigana. Lakini ninyi pia hamna hatia kwa kuwapa wao binti zenu kuwa wake.’ ”

23Basi hivyo ndivyo Wabenyamini walivyofanya. Wakati wasichana walipokuwa wakicheza, kila mtu akamkamata msichana mmoja akamchukua akaenda naye ili awe mke wake. Kisha wakarudi katika urithi wao na kuijenga upya miji na kuishi humo.

24Wakati huo Waisraeli wakaondoka sehemu ile na kwenda nyumbani kwao, kwenye makabila yao na kwa jamaa zao, kila mmoja kwenye urithi wake mwenyewe.

25Katika siku hizo kulikuwa hakuna mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya kile alichoona ni sawa machoni pake mwenyewe.

Copyright information for Neno