Lamentations 4

4:0 Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22
Jinsi dhahabu ilivyopoteza mng'ao wake,
dhahabu iliyo safi imekuwa haing'ai!
Vito vya thamani vimetawanywa
kwenye mwanzo wa kila barabara.
Jinsi wana wa Sayuni wenye thamani,
ambao mwanzo uzito wa thamani yao
ulikuwa wa dhahabu,
sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo,
kazi ya mikono ya mfinyanzi!
Hata mbweha hutoa matiti yao
kunyonyesha watoto wao,
lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma
kama mbuni katika jangwa.
Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga
umegandamana na kaakaa la kinywa chake,
watoto huomba mkate,
lakini hakuna ye yote awapaye.
Wale waliokula vyakula vya kifahari
ni maskini barabarani.
Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau
sasa wanalala kwenye malundo ya majivu.
Adhabu ya watu wangu
ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,
ambayo ilipinduliwa ghafula
bila kuwepo mkono wa kumsaidia.
Wakuu wao walikuwa wameng'aa kuliko theluji
na weupe kuliko maziwa,
miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,
kuonekana kwao kama yakuti samawi.
Lakini sasa ni weusi kuliko masizi;
hawatambulikani barabarani.
Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,
imekuwa mikavu kama fimbo.
Wale waliouawa kwa upanga ni bora
kuliko wale waliokufa kwa njaa;
waliteseka kwa njaa, walitokomea
kwa ajili ya kukosa chakula
kutoka shambani.
10 Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma
walipika watoto wao wenyewe,
ambao walikuwa chakula chao
wakati watu wangu walipoangamizwa.
11 BWANA ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;
ameimwaga hasira yake kali.
Amewasha moto katika Sayuni
ambao umeteketeza misingi yake.
12 Wafalme wa dunia hawakuamini,
wala hapakuwepo mtu ye yote wa duniani,
kwamba adui na watesi wangeweza kuingia
kwenye malango ya Yerusalemu.
13 Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,
na maovu ya makuhani wake,
ambao walimwaga pamoja naye
damu ya wenye haki.
14 Sasa wanapapasa papasa barabarani
kama watu ambao ni vipofu.
Wamenajisiwa kabisa kwa damu
kwamba hakuna ye yote
anayethubutu kugusa mavazi yao.
15 Watu waliwapigia kelele wakisema, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!
Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”
Walipokimbia na kutangatanga huko na huko,
watu miongoni mwa mataifa walisema,
“Hawawezi kukaa hapa zaidi.”
16 BWANA mwenyewe amewatawanya;
hawaangalii tena.
Makuhani hawaonyeshwi heshima,
wazee hawakubaliki.
17 Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,
kwa kutazamia bure msaada;
tuliangalia kutoka minara yetu
kwa taifa lile lisiloweza kutuokoa.
18 Watu walitunyemelea katika kila hatua
kwa hiyo hatukuweza kutembea
katika barabara zetu.
Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,
kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.
19 Waliotufuatia walikuwa wepesi
kuliko tai katika anga;
walitusaka juu milimani
na kutuvizia jangwani.
20 Mpakwa mafuta wa BWANA, pumzi ya uhai wetu hasa,
alinaswa katika mitego yao.
Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake
tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa.
21 Shangilia na ufurahi, Ee Binti Edomu,
wewe ambaye unaishi katika nchi ya Usi.
Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,
Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.
22 Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha,
hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni.
Lakini, Ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako
na atafunua uovu wako.
Copyright information for Neno