Lamentations 5

Kumbuka, Ee BWANA, yaliyotupata,
tazama, nawe uione aibu yetu.
Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni,
na nyumba zetu kwa wageni.
Tumekuwa yatima wasio na baba,
mama zetu wamekuwa kama wajane.
Ni lazima kununua maji tunayokunywa,
kuni zetu zinaweza kupatikana tu kwa kununua.
Wale ambao wanatufuatilia wapo kwenye visigino vyetu,
tumechoka na hakuna pumziko.
Tumejitolea kwa Misri na Ashuru
tupate chakula cha kutosha.
Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena,
na sisi tunachukua adhabu yao.
Watumwa wanatutawala
na hakuna ye yote wa kutuweka huru kutoka katika mikono yao.
Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu
kwa sababu ya upanga jangwani.
10 Ngozi yetu ina joto kama jiko la kuokea,
kwa sababu ya fadhaa itokanayo na njaa.
11 Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni,
na mabikira katika miji ya Yuda.
12 Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao,
wazee hawapewi heshima.
13 Vijana wanaume wanataabika kwenye mawe ya kusagia,
wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni.
14 Wazee wameondoka toka lango la mji,
vijana wa kiume wameacha kuimba kwa vinanda vyao.
15 Furaha imeondoka katika mioyo yetu,
kucheza kwetu kumegeuka maombolezo.
16 Taji imeanguka kutoka kichwani petu.
Ole wetu, kwa maana tumetenda Dhambi!
17 Kwa sababu ya hiyo mioyo yetu inazimia,
kwa sababu ya mambo haya macho yetu yamefifia,
18 kwa ajili ya Mlima Sayuni, ambao unakaa ukiwa,
mbweha huzungukazunguka juu yake.
19 Wewe, Ee BWANA tawala milele,
kiti chako cha enzi chadumu kutoka kizazi mpaka kizazi.
20 Kwa nini watusahau siku zote?
Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu?
21 Uturudishe kwako mwenyewe, Ee BWANA,
ili tupate kurudi;
zifanye mpya siku zetu kama siku za kale,
22 labda uwe umetukataa kabisa
na umetukasirikia pasipo kipimo.
Copyright information for Neno