Leviticus 11

Vyakula Najisi Na Visivyo Najisi

BWANA akawaambia Mose na Aroni, “Waambie Waisraeli: ‘Kati ya wanyama wote waishio juu ya nchi, hawa ndio mtakaowala: Mwaweza kula mnyama ye yote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua.

“ ‘Kuna wanyama wengine ambao hucheua tu au wenye kwato zilizogawanyika tu, lakini hao kamwe msiwale. Ngamia, ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; kwa kawaida ya ibada hiyo ni najisi kwenu. Pelele, ingawa hucheua, lakini hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu. Sungura, ingawa hucheua lakini hana kwato zilizogawanyika; ni najisi kwenu. Naye nguruwe ingawa anazo kwato zilizogawanyika sehemu mbili, lakini hacheui; ni najisi kwenu. Kamwe msile nyama yao wala kugusa mizoga yao; wao ni najisi kwenu.

“ ‘Kuhusu viumbe vyote vinavyoishi ndani ya maji ya bahari na vijito, mtakula wale wote wenye mapezi na magamba. 10 Lakini viumbe vyote ndani ya bahari au vijito visivyo na mapezi na magamba, vikiwa miongoni mwa makundi au viumbe vyote ndani ya maji, hivyo ni machukizo kwenu. 11 Navyo vitakuwa machukizo kwenu. Msile nyama yao, nayo mizoga yao itakuwa machukizo. 12 Cho chote kinachoishi ndani ya maji ambacho hakina mapezi na magamba kitakuwa chukizo kwenu.

13 “ ‘Wafuatao ndio ndege watakaokuwa machukizo kwenu, hivyo msiwale kwa sababu ni chukizo: tai, furukombe, kipungu, 14 mwewe mwekundu, aina zote za mwewe mweusi, 15 aina zote za kunguru, 16 mbuni, kirukanjia, dudumizi, kipanga, shakwe, aina zote za mwewe, 17 bundi, mnandi, bundi mkubwa, 18 mumbi, mwari, mderi, 19 korongo, aina zote za koikoi, hudihudi na popo.

20 “ ‘Wadudu wote warukao wale watembeao kwa miguu minne watakuwa chukizo kwenu. 21 Lakini, wako viumbe wenye mabawa ambao hutembea kwa miguu minne mtakaowala: wale wenye vifundo katika miguu yao ya kurukaruka juu ya ardhi. 22 Miongoni mwa hawa, mtakula nzige wa aina zote, senene, parare au panzi. 23 Lakini viumbe wengine wote wenye mabawa na wenye miguu minne ni machukizo kwenu.

Wanyama Ambao Ni Najisi

24 “ ‘Wanyama hawa watawanajisi ninyi. Ye yote agusaye mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 25 Ye yote atakayebeba mizoga ya viumbe hawa ni lazima afue nguo zake naye atakuwa najisi mpaka jioni.

26 “ ‘Kila mnyama mwenye ukwato ulioachana lakini haukugawanyika kabisa au yule asiyecheua ni najisi kwenu; ye yote atakayegusa mzoga wo wote wa hao atakuwa najisi. 27 Miongoni mwa wanyama wote watembeao kwa miguu minne, wale watembeao kwa vitanga vyao ni najisi kwenu; ye yote atakayegusa mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 28 Ye yote atakayebeba mizoga yao ni lazima afue nguo zake na atakuwa najisi mpaka jioni. Wanyama hawa ni najisi kwenu.

29 “ ‘Kuhusu wanyama watambaao juu ya ardhi, hawa ni najisi kwenu: kicheche, panya, aina yo yote ya mijusi mikubwa, 30 guruguru, kenge, mijusi ya ukutani, goromoe na kinyonga. 31 Hao wote watambaao juu ya ardhi ni najisi kwenu. Ye yote atakayegusa mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 32 Ikiwa mmoja wao atakufa na kuangukia juu ya kitu fulani, chombo hicho, hata kikiwa cha matumizi gani, kitakuwa najisi, kiwe kimetengenezwa kwa mti, nguo, ngozi au gunia. Kiweke ndani ya maji; kitakuwa najisi mpaka jioni, kisha kitakuwa safi tena. 33 Ikiwa mmoja wa wanyama aliyekufa ataangukia ndani ya chungu, kila kilichomo katika chungu hicho kitakuwa najisi, nawe ni lazima uvunje chungu hicho. 34 Chakula cho chote ambacho chaweza kuliwa lakini kikawa kimeingia maji kutoka kwenye chungu hicho ni najisi na kitu cho chote cha majimaji ambacho chaweza kunyweka kutoka kwenye chungu hicho ni najisi. 35 Cho chote ambacho mzoga wa mmojawapo utaangukia kitakuwa najisi, jiko au chungu cha kupikia ni lazima kivunjwe. Ni najisi, nawe ni lazima uvihesabu kuwa najisi. 36 Lakini chemchemi au kisima, mahali pa kuchota maji, patakuwa safi, lakini ye yote atakayegusa moja ya mizoga hii ni najisi. 37 Kama mzoga ukianguka juu ya mbegu zo zote ambazo ni za kupanda, zinabaki safi. 38 Lakini kama mbegu imetiwa maji na mzoga ukaanguka juu yake, hiyo mbegu ni najisi kwenu.

39 “ ‘Kama mnyama ambaye mnaruhusiwa kumla akifa, ye yote atakayeugusa mzoga wake atakuwa najisi mpaka jioni. 40 Ye yote atakayekula sehemu ya mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni. Ye yote atakayebeba mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

41 “ ‘Kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi ni chukizo; kisiliwe. 42 Msile kiumbe cho chote kitambaacho juu ya ardhi, kiwe kitambaacho kwa tumbo lake au kitambaacho kwa miguu minne au kwa miguu mingi; ni chukizo. 43 Msijitie unajisi kwa cho chote katika viumbe hivi. Msijitie unajisi kwa viumbe hivyo na hivyo ninyi wenyewe kuwa najisi. 44 Mimi ndimi BWANA Mungu wenu; jitakaseni mwe watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu. Msijitie unajisi wenyewe kwa kiumbe cho chote kile kiendacho juu ya ardhi. 45 Mimi ndimi BWANA niliyewapandisha mtoke Misri ili niwe Mungu wenu; kwa hiyo iweni watakatifu kwa sababu Mimi ni mtakatifu.

46 “ ‘Haya ndiyo masharti kuhusu wanyama, ndege, kila kiumbe hai kiendacho ndani ya maji na kila kiumbe kiendacho juu ya ardhi. 47 Ni lazima mpambanue kati ya kilicho najisi na kilicho safi, kati ya viumbe hai vinavyoweza kuliwa na vile visivyoweza kuliwa.’ ”

Copyright information for Neno