Leviticus 18

Uhusiano Wa Kukutana Kimwili Kinyume Cha Sheria

1BWANA akamwambia Mose, 2“Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Mimi ndimi BWANA Mungu wenu. 3Msifanye kama wafanyavyo huko Misri, mahali mlipokuwa mnaishi, wala msifanye kama wanavyofanya katika nchi ya Kanaani, mahali ninapowapeleka. Msifuate matendo yao. 4Ni lazima mzitii sheria zangu, nanyi iweni waangalifu kuzifuata amri zangu. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu. 5Mzishike amri zangu na sheria zangu, kwa maana mtu anayezitii ataishi kwa hizo. Mimi ndimi BWANA.

6“ ‘Hakuna mtu awaye yote atakayemsogelea ndugu wa karibu ili kukutana naye kimwili. Mimi ndimi BWANA.

7“ ‘Usimvunjie heshima baba yako kwa kukutana kimwili na mama yako. Yeye ni mama yako; usiwe na mahusiano kama hayo naye.

8“ ‘Usikutane kimwili na mke wa baba yako; hiyo itamvunjia heshima baba yako.

9“ ‘Usikutane kimwili na dada yako, wala binti wa baba yako, au binti wa mama yako, awe amezaliwa katika nyumba hiyo au mahali pengine.

10“ ‘Usikutane kimwili na binti wa mwanao ama binti wa binti yako; utajivunjia heshima.

11“ ‘Usikutane kimwili na binti wa mke wa baba yako, aliyezaliwa na baba yako; huyo ni dada yako.

12“ ‘Usikutane kimwili na dada wa baba yako; ni ndugu wa karibu wa baba yako.

13“ ‘Usikutane kimwili na dada wa mama yako, kwa sababu ni ndugu wa mama yako wa karibu.

14“ ‘Usimvunjie heshima ndugu wa baba yako, kwa kukutana kimwili na mke wake; yeye ni shangazi yako.

15“ ‘Usikutane kimwili na mkwe wako, yeye ni mke wa mwanao; usiwe na mahusiano kama hayo naye.

16“ ‘Usikutane kimwili na mke wa kaka yako; utamvunjia heshima kaka yako.

17“ ‘Usikutane kimwili na mwanamke kisha na binti yake. Usikutane kimwili na binti wa mwanawe au binti wa binti yake; hao ni ndugu zake wa karibu. Huo ni uovu.

18“ ‘Usimchukue dada wa mke wako kuwa mke mwenza na kukutana naye kimwili wakati bado mke wako anaishi.

19“ ‘Usimsogelee mwanamke ili kukutana naye kimwili wakati wa unajisi wa siku zake za mwezi.

20“ ‘Usikutane kimwili na mke wa jirani yako na kujitia naye unajisi.

21“ ‘Usimtoe mtoto wako ye yote awe kafara kwa mungu Moleki, kamwe usilinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi BWANA.

22“ ‘Usikutane kimwili na mwanaume kama mtu akutanaye na mwanamke; hilo ni chukizo.

23“ ‘Usikutane kimwili na mnyama na kujitia unajisi kwake. Mwanamke asijipeleke kwa mnyama ili kukutana naye kimwili; huo ni upotovu.

24“ ‘Msijitie unajisi kwa njia yo yote katika hizi, kwa sababu hivi ndivyo mataifa nitakayoyafukuza mbele yenu yalivyojitia unajisi. 25Hata nchi ikatiwa unajisi, hivyo nikaiadhibu kwa dhambi zake nayo nchi ikawatapika wakazi wake. 26Lakini ni lazima uzitunze amri zangu na sheria zangu. Mzaliwa na wageni waishio miongoni mwenu kamwe wasifanye mambo yo yote ya machukizo haya, 27kwa kuwa mambo haya yote yalifanywa na watu walioishi katika nchi hii kabla yenu na nchi ikawa najisi. 28Kama mkiinajisi nchi, itawatapika kama ilivyowatapika mataifa yaliyowatangulia.

29“ ‘Kila mtu atakayefanya mojawapo ya machukizo haya, watu hao ni lazima wakatiliwe mbali na watu wao. 30Shikeni maagizo yangu, wala msifuate desturi za machukizo yo yote yaliyofanywa kabla hamjafika katika nchi hii na kujitia unajisi kwa hayo. Mimi ndimi BWANA Mungu wako.’ ”

Copyright information for Neno