Leviticus 22

Matumizi Ya Sadaka Takatifu

1BWANA akamwambia Mose, 2“Mwambie Aroni na wanawe kushughulikia kwa uangalifu sadaka takatifu Waisraeli wanazoziweka wakfu kwangu, ili wasilinajisi Jina langu takatifu. Mimi ndimi BWANA.

3“Waambie: ‘Katika vizazi vijavyo, ikiwa ye yote wa wazao wako ni najisi kwa taratibu za kiibada, naye akakaribia sadaka takatifu Waisraeli wanazoziweka wakfu kwa BWANA, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na uso wangu. Mimi ndimi BWANA.

4“ ‘Ikiwa mzao wa Aroni ana ugonjwa wa ngozi unaoambukiza au anatokwa na usaha mwilini, hawezi kula sadaka takatifu mpaka atakasike. Vile vile atakuwa najisi ikiwa atagusa kitu cho chote kilichotiwa unajisi kwa kugusa maiti au mtu aliyetokwa na shahawa, 5au ikiwa atagusa kitu cho chote kitambaacho hicho kimfanyacho mtu najisi, au mtu ye yote awezaye kumtia unajisi, unajisi uwao wote. 6Mtu anayegusa kitu cho chote cha aina hiyo atakuwa najisi mpaka jioni. Kamwe hatakula sadaka yo yote takatifu mpaka yeye mwenyewe awe ameoga kwa maji. 7Wakati jua linapotua, atakuwa safi na baada ya hilo anaweza kula sadaka takatifu, kwa kuwa ni vyakula vyake. 8Kamwe asile nyama ya mzoga wala iliyoraruliwa na wanyama pori, naye akatiwa unajisi kwa hilo. Mimi ndimi BWANA.

9“ ‘Makuhani lazima washike maagizo yangu ili wasiwe na hatia, wakafa kwa kuyadharau. Mimi ndimi BWANA ninayewafanya watakatifu.

10“ ‘Hakuna mtu ye yote asiye wa jamaa ya kuhani anayeruhusiwa kula sadaka takatifu, wala mgeni wa kuhani au mfanyakazi wake haruhusiwi kuila. 11Lakini ikiwa kuhani amenunua mtumwa kwa fedha, au mtumwa amezaliwa katika nyumba ya kuhani huyo, mtumwa huyo aweza kula chakula cha huyo kuhani. 12Ikiwa binti wa kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, binti huyo haruhusiwi kula cho chote cha matoleo matakatifu. 13Lakini ikiwa binti wa kuhani amekuwa mjane au amepewa talaka, naye hana watoto, naye akarudi kuishi na jamaa ya baba yake kama wakati wa usichana wake, binti huyo anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mtu asiyeruhusiwa hawezi kula cho chote katika chakula hiki.

14“ ‘Ikiwa mtu ye yote amekula sadaka takatifu kwa makosa, lazima atoe malipo ya sadaka hiyo kwa kuhani na kuongeza sehemu ya tano ya thamani ya sadaka hiyo. 15Kamwe makuhani wasiinajisi sadaka takatifu ambayo Waisraeli wameitoa kwa BWANA 16kwa kuwaruhusu kuzila sadaka hizo takatifu, na hivyo kuwaletea hatia ya kudaiwa malipo. Mimi ndimi BWANA niwafanyaye watakatifu.’ ”

Dhabihu Zisizokubalika

17BWANA akamwambia Mose, 18“Sema na Aroni, wanawe na Waisraeli wote na uwaambie: ‘Ikiwa mmoja wenu, aliye Mwisraeli au mgeni anayeishi katika nchi ya Israeli, atatoa matoleo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa BWANA, iwe kutimiza nadhiri au kuwa sadaka ya hiari, 19lazima mtoe mnyama dume asiye na dosari akiwa ng'ombe, mbuzi au kondoo ili kwamba aweze kukubalika kwa niaba yako. 20Kamwe usitoe kitu cho chote chenye dosari kwa sababu hakitakubaliwa kwa niaba yako. 21Mtu ye yote aletapo sadaka ya amani kwa BWANA kutoka kundi la ng'ombe au mbuzi ili kutimiza nadhiri maalum au sadaka ya hiari, lazima sadaka hiyo isiwe na dosari au waa ili ikubalike. 22Kamwe usimtolee BWANA mnyama aliye kipofu, aliyejeruhiwa wala aliye kilema, au cho chote kilicho na uvimbe, au chenye upele au vidonda vinavyotoka usaha. Kamwe cho chote cha aina hii kisiwekwe juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa BWANA ya kuteketezwa kwa moto. 23Pengine, waweza kuamua na ukatoa sadaka ya hiari ng'ombe au kondoo mwenye kilema au aliyedumaa, lakini hii haitakubalika ili kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri. 24Kamwe usimtolee BWANA mnyama ambaye mapumbu yake yamejeruhiwa, au aliyehasiwa, au yaliyoraruliwa au kukatwa. Kamwe usifanye katika nchi yako mwenyewe, 25na kamwe usikubali wanyama wa aina hii kutoka katika mkono wa mgeni na kuwatoa wanyama hao kuwa chakula kwa Mungu wako. Wanyama hao hawatakubaliwa kwa niaba yako, kwa sababu wana vilema, nao wana dosari.’ ”

26BWANA akamwambia Mose, 27“Wakati ndama, mwana-kondoo au mwana-mbuzi azaliwapo, atabaki na mama yake kwa siku saba. Kuanzia siku ya nane na kuendelea anaweza kukubaliwa kuwa sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa kuteketezwa kwa moto. 28Usimchinje ng'ombe na ndama wake, au kondoo na kitoto chake siku moja.

29“Unapomtolea BWANA dhabihu ya shukrani, itoe kwa namna ambayo itakubalika kwa niaba yako. 30Ni lazima iliwe siku iyo hiyo, pasipo kubakiza cho chote mpaka asubuhi. Mimi ndimi BWANA.

31“Shikeni maagizo yangu na kuyafuata. Mimi ndimi BWANA. 32Msilinajisi Jina langu takatifu. Lazima nikubalike kuwa mtakatifu kwa Waisraeli. Mimi ndimi BWANA ninayewafanya watakatifu 33na niliyewatoa katika nchi ya Misri niwe Mungu wenu. Mimi ndimi BWANA.”

Copyright information for Neno