Leviticus 23

Sikukuu Zilizoamuriwa

1BWANA akamwambia Mose, 2“Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Hizi ndizo sikukuu zangu zilizoamuriwa, sikukuu zilizoamuriwa za BWANA, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu.

Sabato

3“ ‘Kuna siku sita mnazoweza kufanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, siku ya kusanyiko takatifu. Hamtafanya kazi yo yote, po pote mnapoishi, ni Sabato kwa BWANA.

Pasaka Na Mikate Isiyotiwa Chachu

4“ ‘Hizi ni sikukuu za BWANA zilizoamuriwa, makusanyiko matakatifu mtakayoyatangaza kwa nyakati zilizoamuriwa: 5Pasaka ya BWANA huanza jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. 6Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa kwanza Sikukuu ya BWANA ya Mikate Isiyotiwa Chachu huanza; kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. 7Katika siku ya kwanza mtafanya kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida. 8Kwa siku saba mtamletea BWANA sadaka ya kuteketezwa kwa moto. Kwenye siku hiyo ya saba mtafanya kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida.’ ”

Malimbuko

9BWANA akamwambia Mose, 10“Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi nitakayowapa na kuvuna mazao ya nchi hiyo, leteni kwa kuhani mganda wa mavuno ya kwanza ya nafaka. 11Naye atauinua huo mganda mbele za BWANA ili ukubaliwe kwa niaba yenu; kuhani ataupunga siku inayofuata Sabato. 12Siku hiyo mtakapoinua huo mganda, lazima mtoe kwa BWANA dhabihu ya kuteketezwa kwa moto mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari, 13pamoja na sadaka ya unga laini wa nafaka sehemu mbili za kumi za efa
23.13 Sehemu mbili za kumi za efa ni sawa na kilo mbili
uliochanganywa na mafuta, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kupendeza, na sadaka ya kinywaji robo ya hini
23.13 Robo ya hini ni sawa na lita moja
ya divai.
14Kamwe msile mkate wo wote, au nafaka iliyokaangwa au nafaka mpya, mpaka siku ile mtakayomletea Mungu wako sadaka hii. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo po pote mnapoishi.

Sikukuu Za Majuma

15“ ‘Tangu siku ile iliyofuata Sabato, siku mliyotoa sadaka ya mganda wa kuinuliwa, hesabuni majuma saba kamili. 16Mtahesabu mpaka siku inayofuata Sabato ya saba, siku hamsini, ndipo mtatoa sadaka ya nafaka mpya kwa BWANA. 17Kutoka po pote mnapoishi, leteni mikate miwili iliyookwa kwa unga laini, sehemu mbili za kumi za efa uliookwa wenye chachu, kuwa sadaka ya kuinuliwa ya malimbuko kwa BWANA. 18Toeni pamoja na hiyo mikate wana-kondoo saba, kila mmoja wa mwaka mmoja asiye na dosari, fahali mchanga, na kondoo waume wawili. Watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto iliyotolewa kwa BWANA, pamoja na sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji, sadaka iliyotolewa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. 19Kisha toeni dhabihu mbuzi dume mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili kila mmoja wa mwaka mmoja, kwa ajili ya sadaka ya amani. 20Kuhani atawainua hao wana-kondoo wawili mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa, pamoja na mkate wa malimbuko. Ni sadaka takatifu kwa BWANA kwa ajili ya kuhani. 21Siku iyo hiyo mtatangaza kusanyiko takatifu, na msifanye kazi zenu za kawaida. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo po pote mnapoishi.

22“ ‘Mnapovuna mavuno ya ardhi yenu, msivune hadi mpakani mwa shamba lenu au kukusanya masazo ya mavuno yenu. Hayo utayaacha kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ”

Sikukuu Ya Tarumbeta

23BWANA akamwambia Mose, 24“Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba mtakuwa na siku ya mapumziko, kusanyiko takatifu kwa ukumbusho pamoja na kupigwa kwa tarumbeta. 25Msifanye kazi zenu zo zote za kawaida, lakini toeni sadaka kwa BWANA iliyoteketezwa kwa moto.’ ”

Siku Ya Upatanisho

26BWANA akamwambia Mose, 27“Siku ya kumi ya mwezi huu wa saba ni Siku ya Upatanisho. Mtafanya kusanyiko takatifu, mfunge, nanyi mtoe sadaka kwa BWANA ya kuteketezwa kwa moto. 28Msifanye kazi siku hiyo, kwa sababu ni Siku ya Upatanisho, upatanisho unapofanyika kwa ajili yenu mbele za BWANA Mungu wenu. 29Mtu ye yote ambaye hatafunga siku hiyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. 30Mtu ye yote atakayefanya kazi siku hiyo nitamwangamiza kutoka miongoni mwa watu wake. 31Hamtafanya kazi kamwe. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo po pote mnapoishi. 32Ni Sabato ya mapumziko kwenu ninyi, ni lazima mfunge. Tangu jioni ya siku ya tisa ya mwezi hadi jioni inayofuata, mtaishika Sabato yenu.”

Sikukuu Ya Vibanda

33BWANA akamwambia Mose, 34“Waambie Waisraeli: ‘Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, Sikukuu ya BWANA ya vibanda itaanza, nayo itaadhimishwa kwa siku saba. 35Siku ya kwanza ni kusanyiko takatifu, msifanye kazi zenu za kawaida. 36Kwa siku saba toeni sadaka kwa BWANA za kuteketezwa kwa moto, kwenye siku ya nane fanyeni kusanyiko takatifu na mtoe sadaka kwa BWANA ya kuteketezwa kwa moto. Ni kusanyiko la mwisho, msifanye kazi zenu za kawaida.

37(“ ‘Hizi ni sikukuu za BWANA zilizoamuriwa, ambazo mtazitangaza kuwa makusanyiko matakatifu kwa kuleta sadaka kwa BWANA za kuteketeza kwa moto: sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, dhabihu na sadaka za vinywaji zitahitajika kila siku. 38Sadaka hizi ni nyongeza ya zile mnazozitoa katika Sabato za BWANA, na pia ni nyongeza ya matoleo yenu ya cho chote mlichoweka nadhiri, na sadaka zenu zote za hiari mnazozitoa kwa BWANA.)

39“ ‘Basi kuanzia siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, baada ya kuvuna mazao yote ya nchi, mtaadhimisha sikukuu kwa BWANA kwa siku saba; siku ya kwanza ni mapumziko, pia siku ya nane ni mapumziko. 40Kwenye siku ya kwanza mtachukua matunda mazuri ya miti, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi, na matawi ya mirebi, nanyi mtashangilia mbele za BWANA Mungu wenu kwa siku saba. 41Mtaadhimisha siku hii kuwa sikukuu kwa BWANA kwa siku saba kila mwaka. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo; iadhimisheni kwenye mwezi wa saba. 42Mtaishi katika vibanda kwa siku saba: Wazawa wote wa Waisraeli wataishi katika vibanda, 43ili wazao wenu wajue kuwa niliwafanya Waisraeli waishi kwenye vibanda nilipowatoa Misri. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ”

44Kwa hiyo Mose akawatangazia Waisraeli sikukuu zilizoamuriwa na BWANA.

Copyright information for Neno