Leviticus 24

Mafuta Na Mikate Mbele Za BWANA

1BWANA akamwambia Mose, 2“Waagize Waisraeli wakuletee mafuta safi yaliyokamuliwa ya zeituni kwa ajili ya mwanga ili kwamba taa ziwe zinawaka mfululizo. 3Nje ya pazia la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, Aroni ataziwasha taa mbele za BWANA kuanzia jioni hadi asubuhi kwa mfululizo. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. 4Taa zilizo juu ya kinara cha dhahabu safi mbele za BWANA lazima zihudumiwe mfululizo.

5“Chukua unga laini na uoke mikate kumi na miwili, ukitumia sehemu mbili za kumi za efa
24.5 Sehemu mbili za kumi za efa ni sawa na kilo mbili
za unga kwa kila mkate.
6Iweke katika mistari miwili, kila mstari mikate sita, uiweke mbele za BWANA juu ya meza iliyotengenezwa kwa dhahabu safi. 7Kando ya kila mstari weka uvumba safi kama sehemu ya ukumbusho ili kuwakilisha mikate kuwa sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa kuteketezwa kwa moto. 8Mikate hii itawekwa mbele za BWANA kila wakati, Sabato baada ya Sabato, kwa niaba ya Waisraeli, kuwa Agano la kudumu. 9Hii ni mali ya Aroni na wanawe, watakaoila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni sehemu takatifu sana ya fungu lao la kawaida la sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa kuteketezwa kwa moto.”

Mwenye Kukufuru Apigwa Mawe

10Basi mwana wa mama wa Kiisraeli ambaye baba yake ni Mmisri alikwenda miongoni mwa Waisraeli na mapigano yakatokea ndani ya kambi kati yake na Mwisraeli. 11Huyu mwana wa mwanamke wa Kiisraeli akalikufuru Jina la BWANA na kulaani; kwa hiyo wakamleta kwa Mose. (Jina la mama yake aliitwa Shelomithi binti wa Dibri wa kabila la Dani.) 12Nao wakamweka mahabusu mpaka mapenzi ya BWANA yatakapokuwa wazi kwao.

13Ndipo BWANA akamwambia Mose: 14“Mchukue huyo aliyekufuru nje ya kambi. Wale wote waliomsikia akikufuru wataweka mikono juu ya kichwa chake, kisha kusanyiko lote litampiga mawe. 15Waambie Waisraeli: ‘Ikiwa mtu ye yote atamlaani Mungu wake, atakuwa na hatia kwa uovu wake; 16ye yote atakayekufuru Jina la BWANA ni lazima auawe. Kusanyiko lote litampiga kwa mawe. Iwapo ni mgeni au mzawa, atakapolikufuru Jina la BWANA, ni lazima auawe.

17“ ‘Kama mtu ye yote atamwua mtu mwingine, ni lazima auawe. 18Mtu ye yote auaye mnyama wa mtu mwingine lazima afidie, uhai kwa uhai. 19Ikiwa mtu ye yote atamjeruhi jirani yake, cho chote alichomtenda naye atatendewa: 20iwapo amemvunja mfupa atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kama alivyomjeruhi mwenzake, vivyo hivyo ndivyo atakavyojeruhiwa. 21Ye yote auaye mnyama wa mtu lazima alipe fidia, lakini ye yote auaye mtu, lazima auawe. 22Mtakuwa na sheria iyo hiyo kwa mgeni na kwa mzawa. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.’ ”

23Kisha Mose akasema na Waisraeli, nao wakamchukua yule aliyekufuru nje ya kambi na kumpiga mawe. Waisraeli wakafanya kama BWANA alivyomwagiza Mose.

Copyright information for Neno