Leviticus 3

Sadaka Ya Amani

1“ ‘Kama sadaka ya mtu ni sadaka ya amani, naye akatoa ng'ombe kutoka katika kundi, akiwa dume au jike, atamleta huyo mbele za BWANA mnyama asiye na dosari. 2Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka yake na kumchinja penye ingilio la Hema la Kukutania. Ndipo makuhani wana wa Aroni watanyunyiza damu yake pande zote za madhabahu. 3Kutoka kwenye hiyo sadaka ya amani ataleta sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto: mafuta yote ya mnyama yafunikayo sehemu za ndani, ama yanayoungana na hizo sehemu za ndani, 4figo zote pamoja na mafuta yote yanayozizunguka karibu na kiuno na yale yanayofunika ini, ambayo atayaondoa pamoja na figo. 5Kisha wana wa Aroni wataiteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa iliyoko juu ya kuni zinazowaka, kama sadaka ya kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza BWANA.

6“ ‘Kama akitoa kondoo au mbuzi kutoka katika kundi kama sadaka ya amani kwa BWANA, atamtoa dume au jike asiye na dosari. 7Kama akimtoa mwana-kondoo, atamleta mbele za BWANA. 8Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka yake naye atamchinja mbele ya Hema la Kukutania. Kisha wana wa Aroni watanyunyiza damu yake kwenye madhabahu pande zote. 9Kutoka kwenye hiyo sadaka ya amani ataleta dhabihu iliyotolewa kwa BWANA kwa moto: mafuta yake, mafuta yote ya mkia uliokatwa karibu na uti wa mgongo, mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani au yale yanayounganika nazo, 10figo mbili pamoja na mafuta yanayozizunguka yaliyo karibu na kiuno na yale yanayofunika ini, ambayo atayatoa pamoja na figo. 11Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu kama chakula, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto.

12“ ‘Kama sadaka yake ni mbuzi, ataileta mbele za BWANA. 13Ataweka mkono wake juu ya kichwa chake na kumchinja mbele ya Hema la Kukutania. Kisha wana wa Aroni watanyunyiza damu yake kwenye madhabahu pande zote. 14Kutokana na ile sadaka anayotoa, atatoa sadaka hii kwa BWANA kwa moto: mafuta yote yanayofunika sehemu za ndani na yale yanayoungana nazo, 15figo zote mbili pamoja na mafuta yaliyo juu yake karibu na kiuno na yanayofunika ini, ambayo atayaondoa pamoja na figo. 16Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu kama chakula, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri. Mafuta yote ya mnyama ni ya BWANA.

17“ ‘Hii ni kanuni ya kudumu kwa vizazi vijavyo, po pote muishipo: Msile mafuta yo yote ya mnyama wala damu.’ ”

Copyright information for Neno