Leviticus 7

Sadaka Ya Hatia

1“ ‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya hatia, ambayo ni takatifu sana: 2Sadaka ya hatia itachinjiwa mahali pale ambapo sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa, damu yake itanyunyizwa pande zote za madhabahu. 3Mafuta yake yote yatatolewa sadaka: mafuta ya mkia na mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani, 4figo zote mbili pamoja na mafuta yanayozizunguka yaliyo karibu na kiuno na yale yanayofunika ini, ambayo yataondolewa pamoja na hizo figo. 5Kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. Hii ni sadaka ya hatia. 6Mwanaume ye yote katika jamaa ya kuhani aweza kuila, lakini lazima iliwe mahali patakatifu, ni takatifu sana.

7“ ‘Sheria hii ya sadaka ya hatia ni sawa sawa na ile ya sadaka ya dhambi: Nyama ya yule mnyama aliyetolewa sadaka ni ya yule kuhani anayesimamia ibada ya upatanisho. 8Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya ye yote anaweza kuichukua ile ngozi ya mnyama yule aliyetolewa iwe yake. 9Kila sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni au kupikwa katika sufuria au katika kikaangio itakuwa ya kuhani anayeitoa 10na kila sadaka ya nafaka, ikiwa imechanganywa na mafuta au kavu, itakuwa ya wana wa Aroni, nayo itagawanywa sawa.

Sadaka Ya Amani

11“ ‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya amani ambayo mtu aweza kuileta kwa BWANA:

12“ ‘Ikiwa mtu atatoa sadaka ya amani kwa ajili ya kuonyesha shukrani, ndipo pamoja na sadaka hii ya shukrani, atatoa maandazi yasiyotiwa chachu yaliyochanganywa na mafuta, mikate myembamba isiyotiwa chachu iliyopakwa mafuta, maandazi ya unga laini uliokandwa vizuri na kuchanganywa na mafuta. 13Pamoja na sadaka hii ya amani ya shukrani ataleta sadaka ya maandazi yaliyotengenezwa kwa chachu. 14Ataleta moja ya kila aina ya andazi kama sadaka, matoleo kwa BWANA; hii ni ya kuhani anayenyunyiza damu ya sadaka ya amani. 15Nyama ya sadaka ya amani kwa ajili ya shukrani lazima iliwe siku iyo hiyo inapotolewa; hutabakiza kitu cho chote mpaka asubuhi.

16“ ‘Lakini kama sadaka yake ni kwa ajili ya nadhiri au ni sadaka ya hiari, sadaka hiyo italiwa siku hiyo inapotolewa, lakini cho chote kinachobakia kinaweza kuliwa kesho yake. 17Nyama yo yote ya sadaka inayobaki mpaka siku ya tatu lazima iteketezwe kwa moto. 18Kama nyama yo yote ya sadaka ya amani italiwa siku ya tatu, BWANA hataikubali. Haitahesabiwa kwake huyo aliyeitoa, kwa kuwa ni najisi, mtu atakayekula sehemu yake yo yote atakuwa na hatia kwa uovu huo.

19“ ‘Nyama ile inayogusa cho chote ambacho ni najisi kwa kawaida ya ibada kamwe haitaliwa, ni lazima iteketezwe kwa moto. Kuhusu nyama nyingine, mtu ye yote aliye safi kwa kawaida ya ibada anaweza kuila. 20Lakini kama mtu ye yote ni najisi akila nyama yo yote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa BWANA, huyo mtu atakatiliwa mbali na watu wake. 21Kama mtu ye yote akigusa kitu kilicho najisi, ikiwa ni uchafu wa mwanadamu, au mnyama najisi, au kitu cho chote kilicho najisi, kitu cha kuchukiza, kisha akala nyama yo yote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa BWANA, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”

Kula Mafuta Na Kunywa Damu Kwakatazwa

22BWANA akamwambia Mose, 23“Waambie Waisraeli: ‘Msile mafuta yo yote ya ng'ombe, kondoo wala mbuzi. 24Mafuta ya mnyama aliyekutwa amekufa au ameraruliwa na mnyama pori yanaweza kutumika kwa kazi nyingine yo yote, lakini kamwe msiyale. 25Mtu ye yote alaye mafuta ya mnyama ambaye ametolewa sadaka kwa BWANA kwa moto ni lazima akatiliwe mbali na watu wake. 26Po pote mtakapoishi, kamwe msinywe damu ya ndege ye yote wala ya mnyama. 27Ikiwa mtu ye yote atakunywa damu, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.’ ”

Fungu La Makuhani

28BWANA akamwambia Mose, 29“Waambie Waisraeli: ‘Mtu ye yote aletaye sadaka ya amani kwa BWANA ataleta sehemu ya sadaka hiyo kama dhabihu yake kwa BWANA. 30Kwa mikono yake mwenyewe ataileta sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto; ataleta mafuta ya huyo mnyama pamoja na kidari, naye atainua hicho kidari mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa. 31Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Aroni na wanawe. 32Paja la kulia la sadaka zako za amani utampa kuhani kama matoleo. 33Mwana wa Aroni atoaye damu na mafuta ya sadaka ya amani, ndiye atakayepewa paja hilo la kulia kuwa fungu lake. 34Kutoka kwenye sadaka za amani za Waisraeli, mimi Mungu nimepokea kidari kile kilichoinuliwa pamoja na lile paja lililotolewa, nami nimevitoa kwa kuhani Aroni na wanawe kuwa fungu lao la kawaida kutoka kwa Waisraeli.’ ”

35Hii ndiyo sehemu ya sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto ambazo zilitengwa kwa ajili ya Aroni na wanawe siku ile walipowekwa wakfu kumtumikia BWANA katika kazi ya ukuhani. 36Siku ile walipotiwa mafuta, BWANA aliagiza kwamba Waisraeli wawape hili kama fungu lao la kawaida kwa vizazi vijavyo.

37Basi haya ndiyo masharti kuhusu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka, sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia, sadaka ya kuwekwa wakfu na sadaka ya amani, 38ambayo BWANA alimpa Mose juu ya mlima Sinai siku ile alipowaagiza Waisraeli walete sadaka zao kwa BWANA, katika Jangwa la Sinai.

Copyright information for Neno