Leviticus 8

Kuwekwa Wakfu Kwa Aroni Na Wanawe

1BWANA akamwambia Mose, 2“Mletee Aroni na wanawe mavazi yao, mafuta ya upako, fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kondoo waume wawili na kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, 3kisha kusanya mkutano wote kwenye ingilio la Hema la Kukutania.” 4Mose akafanya kama BWANA alivyomwagiza, mkutano ukakusanyika kwenye ingilio la Hema la Kukutania.

5Mose akaliambia kusanyiko, “Hili ndilo BWANA aliloagiza lifanyike.” 6Kisha Mose akamleta Aroni na wanawe mbele, akawaosha kwa maji. 7Akamvika Aroni koti, akamfunga mshipi, akamvika joho na kumvalisha kisibau. Pia akafunga kisibau juu yake na kukifunga kiunoni mwake kwa mshipi wake uliosokotwa kwa ustadi. 8Akaweka kifuko cha kifuani juu yake, na kuweka Urimu na Thumimu
8.8 Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha Kuhani Mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha
kwenye hicho kifuko.
9Kisha akamvika Aroni kilemba kichwani pake, akaweka lile bamba la dhahabu, ile taji takatifu, upande wa mbele wa kilemba, kama BWANA alivyomwagiza Mose.

10Ndipo Mose akachukua mafuta ya upako na kuipaka maskani na kila kitu kilichokuwamo ndani yake, kisha akaviweka wakfu. 11Akanyunyiza baadhi ya mafuta juu ya madhabahu mara saba, akiipaka madhabahu mafuta na vyombo vyake vyote pamoja na sinia na kinara chake, ili kuviweka wakfu. 12Akamimina sehemu ya hayo mafuta ya upako kichwani mwa Aroni, akamtia mafuta ili kumweka wakfu. 13Kisha akawaleta wana wa Aroni mbele, akawavika makoti, akawafunga mishipi na kuwavika vilemba kama BWANA alivyomwagiza Mose.

14Kisha akamtoa fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nao Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 15Mose akamchinja yule fahali na akachukua sehemu ya hiyo damu, kisha kwa kidole chake akaitia kwenye pembe zote za madhabahu ili kuitakasa madhabahu. Akaimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu, kwa hiyo akaiweka wakfu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu. 16Pia Mose akachukua mafuta yote yanayozunguka sehemu za ndani, mafuta yanayofunika ini, figo zote mbili na mafuta yake na kuyateketeza juu ya madhabahu. 17Lakini fahali pamoja na ngozi yake na nyama yake na sehemu zake za ndani na matumbo akayateketeza nje ya kambi, kama BWANA alivyomwagiza Mose.

18Kisha Mose akamleta kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 19Ndipo Mose akamchinja yule kondoo dume na kunyunyiza damu yake pande zote za ile madhabahu. 20Akamkata yule kondoo dume vipande vipande na kukiteketeza kichwa, vile vipande na yale mafuta. 21Kisha akamsafisha sehemu za ndani na miguu kwa maji na kumteketeza yule kondoo dume mzima juu ya madhabahu kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kumpendeza, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto, kama BWANA alivyomwagiza Mose.

22Kisha akaleta kondoo dume mwingine, ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu, Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 23Mose akamchinja yule kondoo dume na kuichukua sehemu ya damu yake na kuipaka juu ya ncha ya sikio la kuume la Aroni na juu ya kidole gumba cha mkono wa kuume na juu ya kidole kikubwa cha mguu wa kuume. 24Pia Mose akawaleta hao wana wa Aroni mbele na kuipaka sehemu ya hiyo damu kwenye ncha za masikio yao ya kuume, juu ya vidole gumba vya mikono ya kuume na juu ya vidole vikubwa vya miguu ya kuume. Kisha akanyunyiza damu pande zote za madhabahu. 25Akachukua mafuta ya mnyama: mafuta ya mkia, mafuta yote yanayozunguka sehemu za ndani, mafuta yanayofunika ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake na paja la kulia. 26Kisha kutoka kwenye kikapu cha mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichokuwa mbele za BWANA, akachukua andazi moja, na jingine lililotengenezwa kwa mafuta, na mkate mwembamba; akaviweka hivi vyote juu ya mafungu ya mafuta ya mnyama na juu ya lile paja la kulia. 27Akaviweka hivi vyote mikononi mwa Aroni na wanawe, na kuviinua mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa. 28Kisha Mose akavichukua kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kuwa sadaka ya kuwekwa wakfu, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa BWANA kwa moto. 29Kisha akachukua kidari, kilicho fungu la Mose la kondoo dume kwa ajili ya kuwekwa wakfu, na kukiinua mbele za BWANA kama sadaka ya kuinuliwa, kama BWANA alivyomwagiza Mose.

30Kisha Mose akachukua sehemu ya mafuta ya upako, sehemu ya damu kutoka kwenye madhabahu na kuvinyunyiza juu ya Aroni na mavazi yake, na juu ya wanawe na mavazi yao. Kwa hiyo akamweka Aroni na mavazi yake wakfu, pamoja na wanawe na mavazi yao.

31Kisha Mose akamwambia Aroni na wanawe, “Pika hiyo nyama kwenye ingilio la Hema la Kukutania na uile hapo pamoja na mkate kutoka kwenye kikapu cha sadaka ya kuweka wakfu, kama nilivyoagiza, nikisema, ‘Aroni na wanawe wataila.’ 32Kisha teketeza nyama na mikate iliyobaki. 33Msitoke kwenye ingilio la Hema la Kukutania kwa muda wa siku saba, mpaka siku zenu za kuwekwa wakfu ziwe zimetimia, kwa kuwa muda wenu wa kuwekwa wakfu utakuwa siku saba. 34Lile lililofanyika leo liliagizwa na BWANA ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu. 35Lazima mkae kwenye ingilio la Hema la Kukutania mchana na usiku kwa siku saba, na kufanya lile BWANA analolitaka, ili kwamba msife; kwa kuwa hilo ndilo nililoamriwa.” 36Kwa hiyo Aroni na wanawe wakafanya kila kitu BWANA alichoamuru kupitia Mose.

Copyright information for Neno