Leviticus 9

Makuhani Waanza Huduma Yao

Katika siku ya nane Mose akawaita Aroni na wanawe na wazee wa Israeli. Akamwambia Aroni, “Chukua ndama dume kwa ajili ya sadaka yako ya dhambi na kondoo dume kwa sadaka yako ya kuteketezwa, wote wawili wasiwe na dosari, nao uwalete mbele za BWANA. Kisha waambie Waisraeli: ‘Chukueni mbuzi dume kwa ajili ya sadaka ya dhambi, ndama na mwana-kondoo, wote wawili wawe wa umri wa mwaka mmoja, wasio na dosari, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa na maksai na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya amani, ili kutoa dhabihu mbele za BWANA, pamoja na sadaka ya nafaka iliyochanganywa na mafuta. Kwa kuwa leo BWANA atawatokea.’ ”

Wakavileta vile vitu Mose alivyowaagiza mbele ya Hema la Kukutania, nalo kusanyiko lote likakaribia na kusimama mbele za BWANA. Ndipo Mose akasema, “Hili ndilo BWANA alilowaagiza mlifanye, ili utukufu wa BWANA upate kuonekana kwenu.”

Mose akamwambia Aroni, “Njoo madhabahuni ili utoe dhabihu yako ya sadaka ya dhambi na sadaka yako ya kuteketezwa, ufanye upatanisho kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili ya watu; kisha utoe sadaka ya upatanisho kwa ajili ya watu, kama vile BWANA alivyoagiza.”

Hivyo Aroni akaja madhabahuni na kumchinja yule ndama kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe. Wanawe wakamletea damu, na akachovya kidole chake katika hiyo damu, akaitia kwenye pembe za madhabahu, damu iliyobaki akaimwaga chini ya madhabahu. 10 Juu ya madhabahu akateketeza mafuta, figo na mafuta yanayofunika ini kutoka kwenye hiyo sadaka ya dhambi, kama BWANA alivyomwagiza Mose, 11 nyama na ngozi akaviteketeza nje ya kambi.

12 Kisha Aroni akachinja sadaka ya kuteketezwa. Wanawe wakamletea damu naye akainyunyiza pande zote za madhabahu. 13 Wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, pamoja na kichwa, naye akaviteketeza juu ya madhabahu. 14 Akasafisha sehemu za ndani na miguu na kuviteketeza juu ya sadaka ya kuteketezwa juu ya madhabahu.

15 Kisha Aroni akaleta sadaka ile iliyokuwa kwa ajili ya watu. Akachukua yule mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, akamchinja na kumtoa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kama alivyofanya kwa ile ya kwanza.

16 Aroni akaleta sadaka ya kuteketezwa na kuitoa kama ilivyoelekezwa. 17 Pia akaleta sadaka ya nafaka, akachukua konzi moja na kuiteketeza juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.

18 Akachinja maksai na kondoo dume kama sadaka ya amani kwa ajili ya watu. Wanawe wakampa ile damu, naye akainyunyiza kwenye madhabahu pande zote. 19 Lakini sehemu zile za mafuta ya yule maksai na kondoo dume, yaani mafuta ya mkia, mafuta yaliyofunika tumbo, ya figo na yaliyofunika ini, 20 hivi vyote wakaviweka juu ya vidari, kisha Aroni akayateketeza hayo mafuta ya wanyama juu ya madhabahu. 21 Aroni akaviinua vile vidari na paja la kulia mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa, kama Mose alivyoagiza.

22 Kisha Aroni akainua mikono yake kuwaelekea watu na kuwabariki. Naye baada ya kutoa dhabihu ya sadaka ya dhambi, sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya amani, akashuka chini.

23 Kisha Mose na Aroni wakaingia kwenye Hema la Kukutania. Walipotoka nje wakawabariki watu; nao utukufu wa BWANA ukawatokea watu wote. 24 Moto ukaja kutoka katika uwepo wa BWANA, ukairamba ile sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sehemu ya mafuta yaliyokuwa juu ya madhabahu. Watu wote walipoona jambo hili, wakapiga kelele kwa furaha na kusujudu.

Copyright information for Neno