Luke 1

1Kwa kuwa, watu wengi wamekaa ili kuandika habari za mambo yaliyotukia katikati yetu, 2kama vile yalivyokabidhiwa kwetu na wale ambao walikuwa mashahidi walioona na watumishi wa Bwana, 3mimi nami baada ya kuchunguza kila kitu kwa uangalifu kuanzia mwanzo, niliamua kukuandikia habari za mambo hayo ewe mtukufu Theofilo, 4ili upate kujua ukweli kuhusu yale uliyofundishwa.

Kuzaliwa Kwa Yohana Mbatizaji Kwatabiriwa

5Wakati wa Herode mfalme wa Uyahudi palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zekaria, ambaye alikuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Aroni. 6Zekaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama. 7Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.

8Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zekaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu, 9alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba. 10Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba.

11Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zekaria. 12Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana akajawa na hofu. 13Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake. 15Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji cho chote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake. 16Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao. 17Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki na kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.”

18Zekaria akamwuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.”

19Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema. 20Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”

21Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zekaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni. 22Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono.

23Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani kwake. 24Baada ya muda si mrefu Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano.

25Akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponiangalia kwa upendeleo na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”

Kuzaliwa Kwa Yesu Kwatabiriwa

26Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti, 27kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria. 28Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!”

29Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?” 30Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu. 31Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume na utamwita jina lake Yesu. 32Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. BWANA Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. 33Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”

34Maria akamwuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”

35Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli, kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. 36Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. 37Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

38Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka akamwacha.

Maria Aenda Kumtembelea Elizabeti

39Wakati huo Maria akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye vilima vya Uyahudi. 40Akaingia nyumbani kwa Zekaria na kumsalimu Elizabeti. 41Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, 42akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45Amebarikiwa yeye aliye amini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.”

Wimbo Wa Maria Wa Sifa

46Naye Maria akasema: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
47nayo roho yangu inamfurahia
Mungu Mwokozi wangu,
48kwa kuwa ameangalia kwa fadhili
unyonge wa mtumishi wake,
hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita mbarikiwa,
49kwa maana yeye Mwenye Nguvu
amenitendea mambo ya ajabu,
jina lake ni takatifu.
50Rehema zake huwaendea wale wamchao,
kutoka kizazi hadi kizazi.
51Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake;
amewatawanya wale wenye kiburi
ndani ya mioyo yao.
52Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya enzi,
lakini amewainua wanyenyekevu.
53Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri
bali matajiri amewafukuza mikono mitupu.
54Amemsaidia mtumishi wake Israeli,
kwa kumbuka ahadi yake ya kumrehemu
55Abrahamu na uzao wake milele,
kama alivyowaahidi baba zetu.”56Maria akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake.

Kuzaliwa Kwa Yohana Mbatizaji

57Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto mwanaume. 58Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye.

59Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zekaria, ambalo ndilo jina la baba yake. 60Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.”

61Wakamwambia, “Hakuna mtu ye yote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.”

62Basi wakamfanyia Zekaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani. 63Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.” 64Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake ukaachiwa, akawa anaongea akimsifu Mungu. 65Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu na katika nchi yote ya vilima vya Uyahudi watu walikuwa wakinena juu ya mambo haya yote. 66Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.

Unabii Wa Zekaria

67Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema: 68“Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.
69Naye ametusimamishia pembe
1.69 Pembe hapa inamaanisha nguvu
ya wokovu
katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,
70kama alivyonena kwa vinywa vya manabii
wake watakatifu tangu zamani,
71kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu
na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:
72ili kuonyesha rehema kwa baba zetu
na kukumbuka Agano lake takatifu,
73kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:
74kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu,
tupate kumtumikia yeye pasipo hofu
75katika utakatifu na haki mbele zake,
siku zetu zote.
76“Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana;
kwa kuwa utamtangulia Bwana
na kuandaa njia kwa ajili yake,
77kuwajulisha watu wake juu ya wokovu
utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,
78kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu,
nuru itokayo juu itatuzukia
79ili kuwaangazia wale waishio gizani
na katika uvuli wa mauti,
kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.”80Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionyesha hadharani kwa Waisraeli.

Copyright information for Neno