Luke 13

Tubu, La Sivyo Utaangamia

Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa. Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo cha namna hiyo wao walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote? La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo. Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu, mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote waliokuwa wanaishi Yerusalemu? Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”

Mfano Wa Mti Usiozaa Matunda

Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja. Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’

“Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea. Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vyema, la sivyo ukate.’ ”

Yesu Amponya Mwanamke Kilema Siku Ya Sabato

10 Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. 11 Wakati uo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyoka wima. 12 Yesu alipomwona, akamwita akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” 13 Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.

14 Lakini mkuu wa sinagogi, akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Kwa hiyo mkuu wa sinagogi akaendelea kuuambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi, katika siku hizo, njoni mponywe, lakini si kuja kuponywa siku ya Sabato.”

15 Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ng'ombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? 16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka katika kifungo hicho siku ya Sabato?”

17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.

Mfano Wa Punje Ya Haradali

18 Kisha Yesu akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini? 19 Umefanana na punje ya haradali ambayo ni ndogo sana, ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti na ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.”

Mfano Wa Chachu

20 Yesu akauliza tena, “Nitaufananisha Ufalme wa Mungu na nini? 21 Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua na kuichanganya kwenye vipimo vitatu
13:21 Ni kama lita 22
vya unga hadi wote ukawa umeumuka.”

Mlango Mwembamba

22 Yesu akapita katika miji na vijiji akifundisha wakati akisafiri kwenda Yerusalemu. 23 Mtu mmoja akamwuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?”

24 Yesu akawaambia, “Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana, nawaambia, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. 25 Wakati mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkigonga mlango na kusema, ‘Bwana, utufungulie mlango.’

“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi wala mtokako.’

26 “Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’

27 “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi wala mtokako. Ondokeni kwangu ninyi watenda maovu!’

28 “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapomwona Abrahamu, Isaki na Yakobo na manabii wote wakiwa katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje. 29 Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika Ufalme wa Mungu. 30 Tazama wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”

Yesu Aomboleza Kwa Ajili Ya Yerusalemu

31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Yesu na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.”

32 Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’ 33 Sina budi kuendelea na safari yangu leo, kesho na kesho kutwa, kwa maana haiwezekani nabii kufa mahali pengine isipokuwa Yerusalemu.

34 “Ewe Yerusalemu, Yerusalemu, wewe uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku akusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, lakini hamkutaka! 35 Tazama nyumba yenu inaachwa ukiwa, ninawaambia hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye katika jina la Bwana.’ ”

Copyright information for Neno