Luke 9

Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili

1Yesu akiisha kuwaita wale kumi na wawili pamoja, aliwapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote, 2kisha akawatuma waende wakahubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa. 3Akawaagiza akisema, “Msichukue cho chote safarini, wala fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala msichukue kanzu ya ziada. 4Katika nyumba yo yote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 5Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kung'uteni mavumbi miguuni mwenu kuwa ushuhuda dhidi yao.” 6Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.

7Basi Herode mtawala wa Galilaya akasikia habari za yote yaliyotendeka, naye akafadhaika kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yohana Mbatizaji amefufuka. 8Wengine wakasema Eliya amewatokea, na wengine wakasema kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka. 9Herode akasema, “Yohana nilimkata kichwa. Lakini ni nani basi huyu ambaye ninasikia habari zake kuhusu mambo kama haya?” Akatamani sana kumwona.

Yesu Awalisha Watu 5,000

10Wale mitume wake waliporudi, wakamweleza Yesu yote waliyofanya. Akawachukua akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida. 11Lakini umati wa watu ulipofahamu alikokwenda, ukamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.

12Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakamjia Yesu na kumwambia, “Uage umati huu wa watu uondoke ili uweze kwenda kwenye vijiji vya karibu na sehemu za jirani, ili kupata chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”

13Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

Wao wakasema, “Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, labda tuende tukanunue chakula cha kuwatosha watu wote hawa.”
14Kwa kuwa walikuwako wanaume wapatao 5,000.

Yesu akawaambia wanafunzi wake, “waketisheni katika makundi ya watu hamsini hamsini.”
15Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. 16Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega, kisha akawapa wanafunzi wake waugawie ule umati wa watu. 17Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyobaki, vikajaa vikapu kumi na viwili.

Petro Amkiri Bwana Yesu Kuwa Ndiye Kristo

18Wakati mmoja, Yesu alipokuwa akiomba faraghani, nao wanafunzi wake wakiwa pamoja naye, akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”

19Wakamjibu, “Wengine husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya na wengine husema, wewe ni mmoja wa nabii wa kale aliyefufuka kutoka kwa wafu.”

20Kisha akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”

Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo
9.20 Yaani Masiya
wa Mungu.”

21Yesu akawakataza wasimwambie mtu ye yote jambo hilo. 22Yesu akasema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, naye atauawa na siku ya tatu atafufuka.”

23Kisha akawaambia wote, “Ye yote anayetaka kunifuata ni lazima ajikane mwenyewe, achukue msalaba wake kila siku na anifuate. 24Kwa maana ye yote atakayekuyaponya maisha yake atayapoteza, lakini ye yote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. 25Je, itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? 26Kama mtu ye yote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea aibu mtu huyo atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu. 27Amin, amin nawaambia, wako baadhi ya watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti mpaka watakapouona Ufalme wa Mungu.”

Bwana Yesu Abadilika Sura

28Yapata siku nane baada ya Yesu kusema hayo, aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana akaenda nao mlimani kuomba. 29Alipokuwa akiomba, mwonekano wa sura yake ukabadilika, mavazi yake yakametameta kama mwanga wa umeme wa radi. 30Ghafula wakawaona watu wawili, Mose na Eliya wakizungumza naye. 31Walionekana katika utukufu wakizungumza na Yesu kuhusu kifo chake ambacho kingetokea huko Yerusalemu. 32Petro na wenzake waliokuwa wamelala usingizi mzito walipoamka, wakaona utukufu wa Yesu na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. 33Mose na Eliya, walipokuwa wanaondoka, Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tukae hapa! Tutajenga vibanda vitatu, kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.” Lakini Petro alikuwa hajui asemacho.

34Alipokuwa bado anazungumza, pakatokea wingu likawafunika, nao wakaogopa walipoingia mle kwenye wingu. 35Sauti ikatoka kwenye lile wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa niliyemchagua, msikilizeni yeye.” 36Baada ya sauti hiyo kusema, walimkuta Yesu akiwa peke yake. Wale wanafunzi wakalihifadhi jambo hili, wala kwa wakati huo hawakumwambia mtu ye yote yale waliyokuwa wameyaona.

Kuponywa Kwa Kijana Mwenye Pepo Mchafu

37Kesho yake, waliposhuka kutoka mlimani, alikutana na umati mkubwa wa watu. 38Mtu mmoja katika ule umati wa watu akapiga kelele, akasema, “Mwalimu, naomba umwangalie mwanangu, ndiye mtoto wangu wa pekee. 39Mara kwa mara pepo mchafu humpagaa na kumfanya apige kelele, kisha humwangusha na kumtia kifafa akatokwa na povu kinywani. Huyo pepo mchafu anamtesa sana na hamwachi ila mara chache. 40Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”

41Yesu akajibu akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka, nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini? Mlete mwanao hapa.”

42Hata yule mtoto alipokuwa akija, yule pepo mchafu akamwangusha, akamtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu amtoke, akamponya yule mtoto, akamrudisha kwa baba yake. 43Watu wote wakastaajabia uweza mkuu wa Mungu. Wakati bado watu wanastaajabia hayo yote aliyokuwa akiyafanya Yesu, yeye akawaambia wanafunzi wake: 44“Sikilizeni kwa makini haya nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu.” 45Lakini wao hawakuelewa alimaanisha nini. Maana ya maneno hayo ilifichika kwao, hivyo hawakuyaelewa, nao wakaogopa kumwuliza maana yake.

Ni Nani Atakayekuwa Mkubwa Kuliko Wote

46Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote. 47Lakini Yesu akayatambua mawazo yao, akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake. 48Kisha akawaambia, “Ye yote atakayemkaribisha mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, atakuwa amenikaribisha mimi na ye yote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma, kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”

49Yohana akasema, “Bwana, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako tukamzuia, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”

50Yesu akasema, “Msimzuie, kwa sababu ye yote ambaye si kinyume nanyi, yu upande wenu.”

Yesu Akataliwa Samaria

51Wakati ulipokaribia wa yeye kuchukuliwa mbinguni, alikaza uso wake kwenda Yerusalemu. 52Akatuma watu wamtangulie, nao wakaenda katika kijiji kimoja cha Samaria kumwandalia kila kitu, 53lakini watu wa kijiji kile hawakumkaribisha kwa sababu alikuwa anakwenda zake Yerusalemu. 54Wanafunzi wake, yaani, Yakobo na Yohana walipoona hayo, wakasema: “Bwana, unataka tuagize moto kutoka mbinguni ili uwaangamize?” 55Yesu akageuka na kuwakemea, 56nao wakaenda kijiji kingine.

Gharama Ya Kumfuata Yesu

57Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata ko kote uendako.”

58Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

59Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.”

Mtu huyo akamjibu, “Bwana, niache kwanza nikamzike baba yangu.”

60Yesu akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.”

61Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikaage jamaa yangu.”

62Yesu akamwambia, “Mtu ye yote atiaye mkono wake kulima, kisha akatazama nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu.”

Copyright information for Neno