Luke 12

Maonyo Dhidi Ya Unafiki

1Wakati huo, umati mkubwa wa watu kwa maelfu, walipokuwa wamekusanyika, hata wakawa wanakanyagana, Yesu akaanza kuzungumza kwanza na wanafunzi wake, akawaambia: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani, unafiki wao. 2Hakuna jambo lo lote lililositirika ambalo halitafunuliwa au lililofichwa ambalo halitajulikana. 3Kwa hiyo, lo lote mlilosema gizani litasikiwa nuruni na kile mlichonong'ona masikioni mkiwa kwenye vyumba vya ndani, kitatangazwa juu ya paa.

4“Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili na baada ya hilo hawawezi kufanya lo lote zaidi. 5Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia mwogopeni huyo! 6Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao. 7Naam, hata idadi ya nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa. Kwa hiyo msiogope, ninyi ni wa thamani kuliko mashomoro wengi.

8“Ninawaambia kwamba, ye yote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu. 9Lakini yeye atakayenikana mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu. 10Naye kila atakaye nena neno baya dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini ye yote atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

11“Watakapowapeleka katika masinagogi mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema: 12Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”

Mfano Wa Tajiri Mpumbavu

13Mtu mmoja katika umati wa watu akamwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane naye urithi wetu.”

14Lakini Yesu akamwambia, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa hakimu wenu au msuluhishi juu yenu?” 15Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”

16Kisha akawaambia mfano huu: “Shamba la mtu mmoja tajiri lilizaa sana. 17Akawaza moyoni mwake, ‘Nifanye nini? Sina mahali pa kuhifadhi mavuno yangu.’

18“Ndipo huyo tajiri akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu za nafaka na kujenga nyingine kubwa zaidi na huko nitayahifadhi mavuno yangu yote na vitu vyangu. 19Nami nitaiambia nafsi yangu, “Nafsi, unavyo vitu vingi vizuri ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi. Pumzika, ule, unywe, ufurahi.” ’

20“Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe! Usiku huu uhai wako unatakiwa. Sasa hivyo vitu ulivyojiwekea akiba vitakuwa vya nani?’

21“Hivyo ndivyo ilivyo kwa wale wanaojiwekea mali lakini hawajitajirishi kwa Mungu.”

Msiwe Na Wasiwasi

22Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo ninawaambia, msisumbukie maisha yenu, kwamba mtakula nini, au miili yenu kwamba mtavaa nini. 23Maisha ni zaidi ya chakula na mwili ni zaidi ya mavazi. 24Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala po pote pa kuhifadhi nafaka, lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni bora kuliko ndege! 25Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kusumbuka anaweza kujiongeza maisha yake hata kwa saa moja? 26Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?

27“Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafumi wala hayasokoti, lakini ninawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote, hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo. 28Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani ambayo leo yapo kesho yanatupwa motoni, si zaidi sana atawavika ninyi enyi wa imani haba! 29Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya. 30Watu wasiomjua Mungu husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote. Naye Baba yenu wa mbinguni anajua kuwa mnavihitaji. 31Bali utafuteni Ufalme wa Mungu na vitu hivyo vyote atawapatia pia.

Utajiri Wa Mbinguni

32“Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwivi hakaribii wala nondo haharibu. 34Kwa maana hazina yako ilipo, ndipo na moyo wako utakapokuwa pia.

Kukesha

35“Iweni tayari mkiwa mmevikwa kwa ajili ya huduma na taa zenu zikiwa zinawaka, 36kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka kwenye karamu ya arusi, ili ajapo na kugonga mlango waweze kumfungulia mara. 37Heri wale watumishi ambao bwana wao atakapokuja atawakuta wakiwa wanakesha. Amin, nawaambia, atajifunga mkanda wake na kuwaketisha ili wale, naye atakuja na kuwahudumia. 38Itakuwa heri kwa watumwa hao ikiwa bwana wao atakapokuja atawakuta wamekesha hata kama atakuja mnamo usiku wa manane, au karibu na mapambazuko. 39Lakini fahamuni jambo hili kwamba: Kama mwenye nyumba angalijua ni saa ipi mwivi atakapokuja, asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. 40Ninyi nanyi imewapasa kuwa tayari saa zote, kwa maana Mwana wa Adamu atakuja saa ambayo hamumtarajii.”

Mtumishi Mwaminifu Na Yule Asiye Mwaminifu

41Ndipo Petro akamwuliza, “Bwana, mfano huu unatuambia sisi peke yetu au watu wote?”

42Yesu akamjibu, “Ni yupi basi wakili mwaminifu na mwenye busara ambaye bwana wake atamfanya msimamizi juu ya nyumba yake yote, naye awape watumishi wengine chakula chao wakati unaofaa? 43Itakuwa ni furaha kwa mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 44Amin nawaambia, atampa mamlaka juu ya vyote alivyo navyo. 45Lakini ikiwa yule mtumishi atawaza moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kurudi,’ akaanza kuwapiga wale watumishi wa kiume na wa kike na kula na kunywa na kulewa, 46bwana wake yule mtumwa atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. Huyo bwana wake atamkata vipande vipande na kumwekea fungu lake pamoja na wale wasio waaminifu.

47“Yule mtumishi anayefahamu vyema mapenzi ya bwana wake na asijiandae wala kufanya kama apendavyo bwana wake, atapigwa kwa mapigo mengi. 48Lakini ye yote ambaye hakujua naye akafanya yale yastahiliyo kupigwa atapigwa kidogo. Ye yote aliyepewa vitu vingi, atadaiwa vingi na ye yote aliyekabidhiwa vingi kwake vitatakiwa vingi.

Sikuleta Amani Bali Mafarakano

49“Nimekuja kuleta moto duniani, laiti kama ungekuwa tayari umewashwa! 50Lakini ninao ubatizo ambao lazima nibatizwe, nayo dhiki yangu ni kuu mpaka ubatizo huo ukamilike! 51Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? La, nawaambia sivyo, nimekuja kuleta mafarakano. 52Kuanzia sasa, kutakuwa na watu watano katika nyumba moja, watatu dhidi ya wawili na wawili dhidi ya watatu. 53Watafarakana baba dhidi ya mwanawe na mwana dhidi ya babaye, mama dhidi ya bintiye na binti dhidi ya mamaye, mama mkwe dhidi ya mkwewe. Naye mkwe dhidi ya mama mkwe wake.”

Kutambua Majira

54Pia Yesu akauambia ule umati wa watu, “Mwonapo wingu likitokea magharibi, mara mwasema, ‘Mvua itanyesha,’ nayo hunyesha. 55Nanyi mwonapo upepo wa kusini ukivuma, ninyi husema, ‘Kutakuwa na joto,’ na huwa hivyo. 56Enyi wanafiki! Mnajua jinsi ya kutambua kuonekana kwa dunia na anga. Inakuwaje basi kwamba mnashindwa kutambua wakati huu wa sasa?

57“Kwa nini hamwamui wenyewe lililo haki? 58Uwapo njiani na adui yako kwenda kwa hakimu, jitahidi kupatana naye mkiwa njiani. La sivyo, atakupeleka kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa afisa, naye afisa atakutupa gerezani. 59Nawaambia, hautatoka humo hadi ulipe senti ya mwisho.”

Copyright information for Neno