Luke 13

Tubu, La Sivyo Utaangamia

1Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa. 2Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo cha namna hiyo wao walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote? 3La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo. 4Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu, mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote waliokuwa wanaishi Yerusalemu? 5Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”

Mfano Wa Mti Usiozaa Matunda

6Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja. 7Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’

8“Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea. 9Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vyema, la sivyo ukate.’ ”

Yesu Amponya Mwanamke Kilema Siku Ya Sabato

10Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. 11Wakati uo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyoka wima. 12Yesu alipomwona, akamwita akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” 13Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.

14Lakini mkuu wa sinagogi, akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Kwa hiyo mkuu wa sinagogi akaendelea kuuambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi, katika siku hizo, njoni mponywe, lakini si kuja kuponywa siku ya Sabato.”

15Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ng'ombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? 16Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka katika kifungo hicho siku ya Sabato?”

17Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.

Mfano Wa Punje Ya Haradali

18Kisha Yesu akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini? 19Umefanana na punje ya haradali ambayo ni ndogo sana, ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti na ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.”

Mfano Wa Chachu

20Yesu akauliza tena, “Nitaufananisha Ufalme wa Mungu na nini? 21Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua na kuichanganya kwenye vipimo vitatu
13:21 Ni kama lita 22
vya unga hadi wote ukawa umeumuka.”

Mlango Mwembamba

22Yesu akapita katika miji na vijiji akifundisha wakati akisafiri kwenda Yerusalemu. 23Mtu mmoja akamwuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?”

24Yesu akawaambia, “Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana, nawaambia, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. 25Wakati mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkigonga mlango na kusema, ‘Bwana, utufungulie mlango.’

“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi wala mtokako.’

26“Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’

27“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi wala mtokako. Ondokeni kwangu ninyi watenda maovu!’

28“Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapomwona Abrahamu, Isaki na Yakobo na manabii wote wakiwa katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje. 29Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika Ufalme wa Mungu. 30Tazama wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”

Yesu Aomboleza Kwa Ajili Ya Yerusalemu

31Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Yesu na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.”

32Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’ 33Sina budi kuendelea na safari yangu leo, kesho na kesho kutwa, kwa maana haiwezekani nabii kufa mahali pengine isipokuwa Yerusalemu.

34“Ewe Yerusalemu, Yerusalemu, wewe uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku akusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, lakini hamkutaka! 35Tazama nyumba yenu inaachwa ukiwa, ninawaambia hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye katika jina la Bwana.’ ”

Copyright information for Neno