Luke 16

Mfano Wa Msimamizi Mjanja

1Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Ilisemekana kwamba huyo msimamizi alikuwa anatumia vibaya mali ya tajiri yake. 2Hivyo huyo tajiri akamwita na kumwuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’

3“Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba. 4Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani kwao.’

5“Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamwuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’

6“Akajibu, ‘Galoni 800
16.6 Galoni 800 ni sawa na lita 4,000
za mafuta ya mizeituni.’

“Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike galoni 400.’

7“Kisha akamwuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’

“Akajibu, ‘Vipimo 1,000
16.7 Vipimo 1,000 ni kama magunia 100
vya ngano.’

“Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, andika vipimo 800!’

8“Yule bwana akamsifu yule msimamizi kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru. 9Nawaambia, tumieni mali ya kidunia kujipatia marafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele.

10“Ye yote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa. 11Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli? 12Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?

13“Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Ama atamchukia mmoja na kumpenda mwingine au atamheshimu mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali
16.13 Mali (au Utajiri) hapa inatoka neno Mamoni kwa Kiaramu au Mamona kwa Kiyunani
.”

14Mafarisayo, ambao walikuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau. 15Yesu akawaambia, “Ninyi mnajifanya kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo.

Sheria Na Ufalme Wa Mungu

16“Torati na manabii vilitumiwa mpaka kuja kwa Yohana Mbatizaji. Tangu wakati huo habari njema za Ufalme wa Mungu zinahubiriwa na kila mmoja hujiingiza kwa nguvu. 17Lakini ni rahisi zaidi mbingu na nchi kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Sheria.

18“Mtu ye yote ampaye mkewe talaka na kumwoa mwanamke mwingine azini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa azini.

Tajiri Na Lazaro

19“Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa, kila siku. 20Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. 21Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kulamba vidonda vyake.

22“Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. 23Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. 24Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’

25“Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. 26Zaidi ya hayo kati yetu na ninyi huko, kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu ye yote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’

27“Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, 28maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.

29“Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Mose na Manabii, wawasikilize hao.’

30“Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’

31“Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na manabii, hawataweza kushawishiwa hata kama atafufuka mtu kutoka kwa wafu.’ ”

Copyright information for Neno