Luke 20

Wahoji Kuhusu Mamlaka Ya Yesu

1Siku moja, Yesu alipokuwa akifundisha watu Hekaluni na kuhubiri habari njema, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, pamoja na wazee wakamjia. 2Wakamwuliza, “Tuambie, unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Ni nani aliyekupa mamlaka haya?”

3Akawajibu, “Nami nitawauliza swali. 4Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

5Wakasemezana wao kwa wao wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ 6Lakini tukisema, ‘ulitoka kwa wanadamu,’ watu wote watatupiga mawe, kwa sababu wanaamini kwamba Yohana alikuwa nabii.”

7Basi wakajibu, “Hatujui ulikotoka.”

8Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.”

Mfano Wa Wapangaji Waovu

9Akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alipanda shamba lake la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10Wakati wa mavuno akamtuma mtumishi wake kwa hao wakulima aliowakodishia ili wampatie sehemu ya mavuno ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima waliokodisha wakampiga na kumfukuza mikono mitupu. 11Akamtuma mtumishi mwingine, huyo naye wakampiga, wakamfanyia mambo ya aibu na kumfukuza. 12Bado akamtuma na mwingine wa tatu, huyu pia wakamjeruhi na kumtupa nje ya shamba.

13“Basi yule mwenye shamba la mizabibu akasema, ‘Nifanye nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa, huenda yeye watamheshimu.’

14“Lakini wale wakulima waliokodisha shamba walipomwona wakasemezana wao kwa wao na kusema, ‘Huyu ndiye mrithi, basi na tumwue ili urithi uwe wetu.’ 15Kwa hiyo wakamtoa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua.”

“Sasa basi yule mwenye shamba la mizabibu atawafanyia nini wakulima hawa waliokodisha shamba?
16Atakuja na kuwaua hao wapangaji na kuwapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.”

Watu waliposikia hayo wakasema, “Mungu apishie mbali jambo hili lisitokee!”

17Lakini Yesu akawakazia macho akasema, “Basi ni nini maana ya yale yaliyoandikwa: “ ‘Jiwe lile walilolikataa waashi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni?’


18Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande na ye yote litakayemwangukia litamsagasaga awe unga.”

19Walimu wa sheria na viongozi wa makuhani wakatafuta njia ya kumkamata mara moja kwa sababu walifahamu kwamba ametoa mfano huo kwa ajili yao. Lakini waliwaogopa watu.

Kumlipa Kaisari Kodi

20Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa waaminifu ili wapate kumtega kwa maneno asemayo ili wamtie katika uwezo na mamlaka ya mtawala. 21Hivyo wale wapelelezi wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu kwa kufuata ukweli. 22Je, ni halali sisi kumlipa Kaisari kodi au la?”

23Lakini Yesu akatambua hila yao, kwa hiyo akawaambia, “Kwa nini ninyi mnanijaribu? 24Nionyesheni dinari. Je, picha hii na maandishi haya yaliyoko juu yake ni ya nani?”

25Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.”

Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari na Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”

26Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu yake, wakanyamaza kimya.

Ufufuo Na Ndoa

27Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumwuliza, 28“Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu wa mtu akifa na kuacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. 29Basi walikuwepo ndugu saba, wa kwanza akaoa, akafa bila kuzaa mtoto. 30Kisha yule wa pili akamwoa huyo mjane, naye akafa bila mtoto. 31Naye wa tatu pia, vivyo hivyo ndugu wote saba wakawa wamemwoa huyo mwanamke na wote wakafa pasipo kupata mtoto. 32Mwishowe, huyo mwanamke mjane naye akafa. 33Sasa basi, siku ya ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani? Maana aliolewa na ndugu wote saba.”

34Yesu akawajibu, “Katika maisha haya watu huoa na kuolewa. 35Lakini wale ambao wamehesabiwa kwamba wanastahili kupata nafasi katika ulimwengu ule na katika ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaolewi. 36Hawa hawawezi kufa tena, kwa maana wao ni kama malaika. Wao ni watoto wa Mungu, kwa sababu ni watoto wa ufufuo. 37Hata Mose alidhihirisha kuwa wafu wanafufuka, kwa habari ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto bila kuteketea, alipomwita Bwana ‘Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo.’ 38Yeye Mungu si Mungu wa wafu bali wa walio hai, kwa kuwa kwake wote ni hai.”

39Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, umesema sawasawa kabisa!”

40Baada ya hayo hakuna mtu aliyethubutu kumwuliza maswali zaidi.

Kristo Ni Mwana Wa Nani?

41Kisha Yesu akawaambia, “Imekuwaje basi wao husema Kristo
20:41 Yaani Masiya
ni Mwana wa Daudi?
42Daudi mwenyewe anasema katika Kitabu cha Zaburi: “ ‘BWANA alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume
43hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’


44Ikiwa Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ basi atakuwaje mwanawe?”

Yesu Awashutumu Walimu Wa Sheria

45Wakati watu wote walipokuwa wanamsikiliza, Yesu akawaambia wanafunzi wake, 46“Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa majoho marefu na kusalimiwa kwa heshima masokoni. Hukaa kwenye viti maalum katika masinagogi na kukaa kwenye sehemu za wageni wa heshima katika karamu. 47Wanakula nyumba za wajane, na ili waonekane mbele ya watu, husali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu.”

Copyright information for Neno