Luke 21

Sadaka Ya Mjane

1Yesu alipoinua macho yake, aliwaona matajiri wakiweka sadaka zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. 2Akamwona pia mwanamke mmoja mjane maskini, akiweka humo sarafu mbili za shaba. 3Yesu akasema, “Amin, amin nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo sadaka kubwa zaidi kuliko wengine wote. 4Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kwa Mungu kutokana na wingi wa mali zao, lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo kwa ajili ya maisha yake.”

Dalili Za Siku Za Mwisho

5Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonyesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Yesu akawaambia, 6“Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalosalia juu ya jiwe jingine, kila moja litabomolewa.”

7Wakamwuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani zitaonyesha kwamba yanakaribia kutendeka?”

8Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai kwamba, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate. 9Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.”

10Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine. 11Kutakuwa na matetemeko ya ardhi katika sehemu mbalimbali, njaa kali na magonjwa ya kuambukiza. Kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.

Mateso

12“Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kufungwa magerezani, nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu. 13Hii itawapa nafasi ya kushuhudia. 14Lakini msiwe na wasiwasi kwamba mtasema nini kabla ya mashtaka. 15Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga. 16Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki na baadhi yenu watawaua. 17Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. 18Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia. 19Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.

Kuharibiwa Kwa Yerusalemu Kwatabiriwa

20“Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia. 21Wakati huo, wale walio Uyahudi wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo na wale walioko mashambani wasiingie mjini. 22Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yote yaliyoandikwa. 23Ole wao wenye mimba na watakaokuwa wananyonyesha katika siku hizo! Kutakuwa na dhiki kuu katika nchi na ghadhabu juu ya hawa watu 24Wataanguka kwa makali ya upanga, wengine watachukuliwa kuwa mateka katika mataifa yote, nao Yerusalemu utakanyagwa na watu Mataifa hadi muda wa hao watu Mataifa utimie.

Kuja Kwa Mwana Wa Adamu

25“Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari. 26Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za vitu vya angani zitatikisika. 27Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu. 28Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”

29Akawaambia mfano huu: “Uangalieni mtini na miti mingine yote. 30Unapochipua majani, ninyi wenyewe mnaweza kuona na kutambua ya kuwa wakati wa kiangazi umekaribia. 31Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yakitukia, mwajua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.

32“Amin, amin nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yatimie. 33Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”

Siku Ya Mwisho Itakuja Ghafula

34“Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo. 35Kwa maana kama vile mtego unasavyo, ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote waishio katika uso wa dunia yote. 36Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.”

37Kila siku Yesu alikuwa akifundisha Hekaluni na jioni ilipofika, alikwenda zake kwenye Mlima wa Mizeituni na kukaa huko usiku kucha. 38Nao watu wote walikuja asubuhi na mapema Hekaluni ili kumsikiliza.

Copyright information for Neno