Luke 22

Yuda Akubali Kumsaliti Yesu

1Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia. 2Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wanatafuta njia ya kumwua Yesu, kwa sababu waliwaogopa watu. 3Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili. 4Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu kuzungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Yesu. 5Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha. 6Naye akakubali, akaanza kutafuta wasaa mzuri wa kumsaliti Yesu kwao wakati ambapo hakuna umati wa watu.

Maandalizi Ya Pasaka

7Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa. 8Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.”

9Wakamwuliza, “Unataka tukuandalie wapi Pasaka?”

10Yesu akawaambia, “Sikilizeni, mtakapokuwa mmeingia mjini, mtakutana na mwanaume mmoja aliyebeba mtungi wa maji, mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia, 11nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza, kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ 12Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, ambacho kina samani zote kikiwa kimepambwa vizuri. Tuandalieni humo.”

13Wakaenda, wakakuta kila kitu kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Kwa hiyo wakaandaa Pasaka.

Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana

14Wakati ulipowadia, Yesu akaketi mezani pamoja na wanafunzi wake. 15Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mungu.”

17Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. 18Kwa maana, nawaambia kwamba, tangu sasa sitakunywa tena divai hadi Ufalme wa Mungu utakapokuja.”

19Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

20Vivyo hivyo baada ya kula, akachukua kile kikombe akasema, “Kikombe hiki ni Agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu. 21Lakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami. 22Mwana wa Adamu anakwenda zake kama ilivyokusudiwa, lakini ole wake mtu huyo atakayemsaliti.” 23Wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni nani miongoni mwetu anayeweza kufanya jambo hilo?

Mabishano Kuhusu Ukuu

24Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani anayeonekana kuwa mkuu wa wote miongoni mwao. 25Yesu akawaambia, “Wafalme na watu wakuu wasiomjua Mungu huwatawala watu wao kwa nguvu na wenye mamlaka juu yao huitwa ‘Wafadhili.’ 26Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye. 27Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumiaye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumiaye. 28Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu. 29Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, kadhalika mimi nami ninawapa ninyi, 30ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu na kukaa katika viti vya enzi, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.”

Yesu Atabiri Kuwa Petro Atamkana

31Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. 32Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”

33Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”

34Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku huu wa leo, utanikana mara tatu kwamba hunijui Mimi.”

Mfuko, Mkoba Na Upanga

35Kisha Yesu akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu cho chote?”

Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu cho chote.”

36Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. 37Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe juu yangu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wahalifu’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu mimi hayana budi kutimizwa.”

38Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.”

Akawajibu, “Inatosha.”

Yesu Aomba Kwenye Mlima Wa Mizeituni

39Yesu akatoka akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata. 40Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni msije mkaangukia majaribuni.” 41Akajitenga nao, kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba, 42akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki, lakini si kama mimi nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.” 43Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu. 44Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.

45Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni. 46Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni mwombe ili msiangukie majaribuni.”

Yesu Akamatwa

47Wakati Yesu alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu ukaja, ukiongozwa na Yuda, ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili. Akamkaribia Yesu ili ambusu. 48Lakini Yesu akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”

49Wafuasi wa Yesu walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?” 50Mmoja wao akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.

51Lakini Yesu akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.

52Kisha Yesu akawaambia viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu na wazee waliokuwa wamekuja, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba Mimi ni mnyang'anyi? 53Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”

Petro Amkana Yesu

54Kisha wakamkamata Yesu, wakamchukua wakaenda naye mpaka nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali. 55Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao. 56Mtumishi mmoja wa kike, kwa kusaidiwa na mwanga wa moto, akamwona Petro ameketi pale. Akamwangalia kwa uangalifu na kusema, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja na Yesu!”

57Lakini Petro akakana akasema, “Ewe mwanamke, hata simjui!”

58Baadaye kidogo, mtu mwingine alimwona Petro akasema, “Wewe pia ni mmoja wao!” Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sio mmoja wao!”

59Baada ya muda wa kama saa moja hivi, mtu mwingine akazidi kusisitiza, “Kwa hakika huyu mtu naye alikuwa pamoja na Yesu, kwa maana yeye pia ni Mgalilaya.”

60Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sijui unalosema!” Wakati uo huo, akiwa bado anazungumza, jogoo akawika. 61Naye Bwana akageuka akamtazama Petro. Ndipo Petro akakumbuka yale maneno ambayo Bwana alimwambia, “Kabla jogoo hajawika leo, utanikana mara tatu.” 62Akatoka nje, akalia sana.

Walinzi Wamdhihaki Yesu Na Kumpiga

63Wale watu waliokuwa wanamlinda Yesu wakaanza kumdhihaki na kumpiga. 64Wakamfunga kitambaa machoni na kumwuliza, “Tabiri! Tuambie ni nani aliyekupiga?” 65Wakaendelea kumtukana kwa matusi mengi.

Yesu Apelekwa Mbele Ya Baraza

66Kulipopambazuka baraza la wazee wa watu
22.66 Baraza la wazee hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo Baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na Kuhani Mkuu
, yaani viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, wakakutana pamoja, naye Yesu akaletwa mbele yao.
67Wakamwambia, “Kama wewe ndiye Kristo
22:67 Yaani Masiya
, tuambie.”

Yesu akawajibu, “Hata nikiwaambia hamtaamini.
68Nami nikiwauliza swali, hamtanijibu. 69Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu ataketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.”

70Wote wakauliza, “Wewe basi ndiwe Mwana wa Mungu?”

Yeye akawajibu, “Ninyi mmesema kwamba Mimi ndiye.”

71Kisha wakasema, “Kwani tunahitaji ushahidi gani zaidi? Tumesikia wenyewe kutoka kinywani mwake.”

Copyright information for Neno