Mark 11

Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Shangwe

1Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni, Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake, 2akiwaambia, “Nendeni kwenye kijiji kilichoko mbele yenu na mara mwingiapo kijijini, mtakuta mwana punda amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote. Mfungueni, mkamlete hapa. 3Kama mtu ye yote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”

4Wakaenda, wakamkuta mwana punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba. 5Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Mna maana gani mnapomfungua huyo mwana punda?” 6Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu. 7Kisha wakamleta huyo mwana punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda. 8Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani. 9Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema, “Hosana
11:9 Kiebrania kusema Okoa, basi likawa neno la shangwe
!”
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana!
10“Umebarikiwa Ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!”
“Hosana kwake yeye aliye juu!”11Yesu akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwemo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.

Yesu Alaani Mtini Usiozaa

12Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa. 13Alipouona mtini kwa mbali, akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. 14Yesu akauambia ule mti, “Tangu leo mtu ye yote na asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.

Yesu Atakasa Hekalu

15Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia Hekaluni akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wananunua na kuuza humo ndani. Akapindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, 16wala hakumruhusu mtu ye yote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. 17Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa: “ ‘Nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote’?


Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyang'anyi.’ ”

18Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumwua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote wa watu walikuwa wanashangazwa na mafundisho yake.

19Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.

Mtini Ulionyauka

20Asubuhi yake, walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. 21Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”

22Yesu akawajibu akawaambia, “Mwaminini Mungu. 23Amin, amin nawaambia, mtu ye yote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. 24Kwa sababu hiyo nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea nayo yatakuwa yenu. 25Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni, mkiwa na neno na mtu ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. 26Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.”

Wauliza Kuhusu Mamlaka Ya Yesu

27Wakafika tena Yerusalemu, wakati Yesu akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamjia. 28Wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Naye ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”

29Yesu akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaeleza ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 30Niambieni, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

31Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ 32Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ ....” (Waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yohana alikuwa nabii kweli kweli.)

33Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatujui.”

Naye Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.”

Copyright information for Neno