Mark 12

Mfano Wa Wapangaji Waovu

Yesu akaanza kusema nao kwa mifano, akawaambia: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akachimba shimo ndani yake kwa ajili ya shinikizo la kusindika divai, akajenga mnara wa ulinzi. Akalikodisha shamba hilo kwa wakulima, kisha akasafiri kwenda nchi nyingine. Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba akamtuma mtumishi wake kwa hao wakulima ili kuchukua sehemu yake ya mavuno kutoka kwa hao wapangaji. Lakini wale wakulima walimkamata yule mtumishi, wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. Kisha yule mwenye shamba akamtuma mtumishi mwingine kwao, wale wakulima wakampiga kichwani na kumfanyia mambo ya aibu. Kisha akatuma mtumishi mwingine, huyu wakamwua. Akatuma wengine wengi, baadhi yao wale wakulima wakawapiga na wengine wakawaua.

“Mwenye shamba alikuwa amebakiwa na mmoja wa kumtuma, huyu ni mwanawe mpendwa. Hatimaye akamtuma akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’

“Lakini wale wapangaji wakasemezana wao kwa wao, wakisema, ‘Huyu ndiye mrithi, njoni tumwue, nao urithi utakuwa wetu.’ Hivyo wakamkamata, wakamwua na kumtupa nje ya lile shamba la mizabibu.

“Mnadhani yule mwenye shamba atafanya nini? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, kisha atawapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu. 10 Je, hamjasoma maandiko haya: “ ‘Jiwe lile walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni;
11 Bwana amefanya jambo hili,
nalo ni ajabu machoni petu’?”12 Walipotambua kuwa amesema mfano huu kwa ajili yao wakataka kumkamata, lakini wakaogopa ule umati wa watu. Wakamwacha wakaondoka, wakaenda zao.

Swali Kuhusu Kulipa Kodi

13 Baadaye wakawatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kuja kumtega Yesu katika yale anayosema. 14 Wakamjia, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua ya kuwa wewe ni mtu mwadilifu. Wewe huyumbishwi na wanadamu, kwa kuwa hujali kwamba wao ni nani. Lakini wewe hulifundisha neno la Mungu sawasawa na kweli. Je, ni haki kumlipa Kaisari kodi au la? 15 Je, tulipe kodi au tusilipe?”

Lakini Yesu alijua unafiki wao. Akawauliza “Mbona mnajaribu kunitega? Nileteeni hiyo dinari
12.15 Dinari moja ilikuwa sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja
niione.”
16 Wakamletea hiyo sarafu. Naye akawauliza, “Picha hii ni ya nani na maandishi haya ni ya nani?”

Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.”

17 Ndipo Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, na kilicho cha Mungu mpeni Mungu.”

Nao wakamstaajabia sana.

Ndoa Wakati Wa Ufufuo

18 Kisha Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wakamjia Yesu, 19 wakasema, “Mwalimu, Mose alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi ndugu yake atamwoa huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto. 20 Basi walikuwapo ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa na akafa pasipo kuwa na mtoto ye yote. 21 Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto ye yote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu. 22 Hakuna hata mmojawapo wa hao ndugu wote saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa. 23 Kwa hiyo wakati wa ufufuo, watakapofufuka wote, huyo atakuwa mke wa nani maana aliolewa na ndugu wote saba?”

24 Yesu akawajibu, “Je, hampotoki kwa sababu hamjui maandiko wala uweza wa Mungu? 25 Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, watakuwa kama malaika wa mbinguni. 26 Basi kuhusu ufufuo wa wafu: Je, hamjasoma katika kitabu cha Mose jinsi Mungu alivyosema na Mose kutoka katika kile kichaka akisema, ‘Mimi, ni Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Isaki na Mungu wa Yakobo?’ 27 Mungu si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Kwa hiyo mmekosea kabisa.”

Amri Iliyo Kuu

28 Mwalimu mmoja wa sheria akaja akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Yesu amewajibu vyema, naye akamwuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”

29 Yesu akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii, ‘Sikia Ee Israeli, Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. 30 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote.’ 31 Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”

32 Yule mwalimu wa sheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja wala hakuna mwingine ila yeye. 33 Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa akili zote na kwa nguvu zote na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora zaidi kuliko kutoa sadaka ya kuteketezwa na dhabihu.”

34 Yesu alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu ye yote aliyethubutu kumwuliza maswali tena.

Kristo Ni Mwana Wa Nani?

35 Wakati Yesu alipokuwa akifundisha Hekaluni, akauliza, “Imekuwaje walimu wa sheria wanasema kwamba Kristo
12:35 Yaani Masiya
ni Mwana wa Daudi?
36 Kwa maana Daudi mwenyewe akinena kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu alisema: “ ‘BWANA alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’


37 Kwa hiyo Daudi mwenyewe anamwita ‘Bwana.’ Awezaje basi yeye kuwa mwanawe?”

Ule umati wote wa watu wakamsikiliza kwa furaha.

Yesu Awatahadharisha Watu Kuhusu Walimu Wa Sheria

38 Alipokuwa akifundisha, Yesu alisema, “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu na kusalimiwa kwa heshima masokoni. 39 Pia wao hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi na kupewa nafasi za heshima katika karamu. 40 Wao hula nyumba za wajane na ili waonekane kuwa wema wanasali sala ndefu. Watapata adhabu iliyo kuu sana.”

Sadaka Ya Mjane

41 Kisha Yesu akaketi mkabala na sehemu sadaka zilikokuwa zinawekwa na kuangalia umati wa watu wakati wakitoa fedha zao kwenye hazina ya Hekalu. Matajiri wengi wakaweka kiasi kikubwa cha fedha. 42 Lakini mjane mmoja maskini akaja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba zenye thamani ya senti mbili.

43 Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Amin, amin, nawaambia, huyu mjane maskini ametoa zaidi katika hazina kuliko wengine wote. 44 Wengine wote wametoa kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mjane kutokana na umaskini wake, ametoa kila kitu alichokuwa nacho, hata kile alichohitaji ili kuishi.”

Copyright information for Neno