Mark 16

Kufufuka Kwa Yesu

Sabato ilipomalizika, Maria Magdalene, Maria mama yake Yakobo na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu. Asubuhi na mapema, siku ya kwanza ya juma, mara tu baada ya kuchomoza jua walikwenda kaburini. Njiani wakawa wanaulizana wao kwa wao, “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe kutoka kwenye ingilio la kaburi?”

Lakini walipotazama, wakaona lile jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana, limekwisha kuvingirishwa kutoka pale penye ingilio la kaburi. Walipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu.

Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulibiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza. Lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba ‘Anawatangulia kwenda Galilaya, huko ndiko mtakakomwona, kama alivyowaambia.’ ”

Hivyo wakatoka wakakimbia kutoka mle kaburini, kwani hofu kuu na mshangao ulikuwa umewapata, nao hawakumwambia mtu ye yote neno lo lote.

[Yesu Anamtokea Maria Magdalene

Yesu alipofufuka alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma alimtokea kwanza Maria Magdalene, yule ambaye alikuwa amemtoa pepo wachafu saba. 10 Maria akaenda akawaambia wale waliokuwa wakifuatana na Yesu, ambao walikuwa wanaomboleza na kulia. 11 Lakini waliposikia kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria alikuwa amemwona, hawakusadiki.

Yesu Awatokea Wanafunzi Wawili

12 Baadaye Yesu akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine. 13 Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia.

Yesu Awaagiza Wale Wanafunzi Kumi Na Mmoja

14 Baadaye Yesu akawatokea wale wanafunzi wake kumi na mmoja, walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutokuamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa sababu hawakuwasadiki wale waliomwona baada ya kufufuka.

15 Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Ye yote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini ye yote asiyeamini atahukumiwa. 17 Nazo ishara hizi zitafuatana na wale waaminio: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu, watasema kwa lugha mpya, 18 watashika nyoka kwa mikono yao na hata wakinywa kitu cho chote cha kuua, hakitawadhuru kamwe, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”

Yesu Apaa Kwenda Mbinguni

19 Baada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu. 20 Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]

Copyright information for Neno