Mark 5

Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo

Wakafika upande wa pili wa bahari wakaingia katika nchi ya Wagerasi. Yesu alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini akakutana naye. Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo, kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa kwa minyororo mikononi na miguuni, akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu ye yote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.

Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia akapiga magoti mbele yake. Akapiga kelele kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” Kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”

Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?”

Akamjibu, “Jina langu ni Legioni
5.9 Legioni maana yake ni Jeshi
, kwa kuwa tuko wengi.”
10 Akamwomba sana Yesu asiwapeleke nje ya nchi ile.

11 Kundi kubwa la nguruwe lilikuwa karibu likilisha kando ya kilima. 12 Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe, turuhusu tuwaingie.” 13 Basi Yesu akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao 2,000, likatelemkia gengeni kwa kasi nalo likazama baharini.

14 Wale waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakatoka kwenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia. 15 Walipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu Legioni, akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na pia akiwa na akili zake timamu. Wakaogopa. 16 Wale walioyaona mambo haya wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule aliyekuwa na pepo wachafu na lile kundi la nguruwe. 17 Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika nchi yao.

18 Yesu alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Yesu waende pamoja. 19 Yesu hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana na jinsi alivyokuhurumia.” 20 Yule mtu akaenda zake akaanza kutangaza katika Dekapoli jinsi Yesu alivyomtendea, nao watu wote wakastaajabu.

Mwanamke Aponywa

21 Yesu alipokwisha kuvuka tena na kufika ng'ambo, umati mkubwa wa watu ukamzunguka, yeye akiwa kando ya bahari. 22 Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi aliyeitwa Yairo, akafika pale, naye alipomwona Yesu akapiga magoti miguuni pake, 23 akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona.” 24 Hivyo Yesu akaenda pamoja naye.

Umati mkubwa wa watu ukamfuata, watu wakawa wanamsonga.
25 Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26 Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi na kutumia kila kitu alichokuwa nacho lakini badala ya kupona hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27 Alikuwa amesikia habari za Yesu naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, 28 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi lake tu, nitapona.” 29 Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.

30 Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyenigusa?”

31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi umati wa watu unavyokusonga, wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”

32 Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa. 33 Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34 Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”

Yesu Amfufua Binti Yairo

35 Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”

36 Kwa kusikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”

37 Hakumruhusu mtu mwingine ye yote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana nduguye Yakobo. 38 Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa. 39 Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa bali amelala tu.” 40 Wale watu wakamcheka kwa dharau.

Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao. Wakaingia ndani mpaka pale alipokuwa yule mtoto.
41 Akamshika mtoto mkono akamwambia, “Talitha koum
5.41 Talitha koum ni lugha ya Kiaramu
!” (Maana yake, “Msichana, ninakuambia, amka!”)
42 Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Walipoona haya, wakastaajabu sana. 43 Yesu akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu ye yote jambo hili, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.

Copyright information for Neno