Mark 6

Nabii Hana Heshima Kwao

1Yesu akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiwa amefuatana na wanafunzi wake. 2Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi na wengi waliomsikia wakashangaa.

Wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!
3Huyu si yule seremala, mwana wa Maria? Na ndugu zake si Yakobo, Yosefu
6.3 Yosefu kwa Kiyunani ni Joses
, Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa petu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake wakakataa kumwamini.

4Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe na miongoni mwa jamaa na ndugu zake.” 5Hakufanya miujiza yo yote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6Naye akashangazwa sana kwa jinsi wasivyokuwa na imani.

Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili

Kisha Yesu akawa anakwenda huku na huko kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha.
7Akawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.

8Akawaagiza akisema, “Msichukue cho chote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu, 9bali mvae viatu, lakini msivae nguo ya ziada.” 10Akawaambia, “Mkiingia kwenye nyumba yo yote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 11Kama mahali po pote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kung'uteni mavumbi yaliyoko miguuni mwenu, ili kuwa ushuhuda dhidi yao.”

12Kwa hiyo wakatoka na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi. 13Wakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya.

Yohana Mbatizaji Akatwa Kichwa

14Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Yesu lilikuwa limejulikana kila mahali. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu ndiyo maana uwezo wa kutenda miujiza unafanya kazi ndani yake!”

15Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”

Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmojawapo wa wale manabii wa zamani.”

16Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yohana Mbatizaji, niliyemkata kichwa, amefufuka!”

17Kwa kuwa Herode alikuwa ameagiza kwamba Yohana Mbatizaji akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo ndugu yake, ambaye alikuwa amemwoa. 18Yohana alikuwa amemwambia Herode, “Si halali wewe kumwoa mke wa ndugu yako.” 19Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yohana kinyongo akataka kumwua. Lakini hakuweza, 20kwa sababu Herode alimwogopa Yohana akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, akawa anamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza.

21Mfalme Herode alifanya karamu kubwa, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. Hatimaye Herodia alipata wasaa aliokuwa akiutafuta. 22Binti yake Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani.

Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu cho chote utakacho, nami nitakupa.”
23Tena akamwahidi kwa kiapo akamwambia, “Cho chote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”

24Yule binti akatoka nje akaenda kumwuliza mama yake, “Niombe nini?”

Mama yake akajibu, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”

25Yule binti akarudi haraka kwa mfalme akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.”

26Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa mbele ya wageni wake hakutaka kumkatalia. 27Mara mfalme akatuma askari mmojawapo wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yohana. Akaenda na kumkata Yohana kichwa humo gerezani, 28akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake. 29Wanafunzi wake walipopata habari hizi, wakaja kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

Yesu Awalisha Watu 5,000

30Wale wanafunzi wa Yesu wakamkusanyikia na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”

32Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao wakaenda mahali pa faragha pasipo na watu. 33Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakawatangulia haraka kwa miguu kutoka katika miji yote, nao wakatangulia kufika. 34Yesu alipofika nchi kavu na kuuona huo umati wa watu, aliwaonea huruma kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mahali hapa ni mbali na pasipo na watu, nazo saa zimekwenda sana. 36Waage watu ili waweze kwenda sehemu za mashambani na vijiji vya jirani, wakajinunulie chakula.”

37Lakini Yesu akawajibu, “Wapeni ninyi chakula.”

Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200
6.37 Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja; hivyo dinari 200 ni sawa na mshahara wa siku 200
ili tuwape watu hawa wale?”

38Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”

Walipokwisha kuona wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”

39Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, 40nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini. 41Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili akatazama mbinguni, akashukuru, kisha akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. 42Watu wote wakala, wakashiba. 43Wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000.

Yesu Atembea Juu Ya Maji

45Mara Yesu akawataka wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye anauaga ule umati wa watu. 46Baada ya kuwaaga wale watu, akaenda mlimani kuomba.

47Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Karibu na mapambazuko, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akitembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, 49lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu, wakapiga yowe, 50kwa sababu wote walipomwona waliogopa.

Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni Mimi, msiogope!”
51Akapanda kwenye mashua yao na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa. 52Kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate, mioyo yao ilikuwa migumu.

53Walipokwisha kuvuka, wakafika Genesareti, wakatia nanga. 54Mara waliposhuka kutoka katika mashua yao, watu wakamtambua Yesu, 55wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali po pote waliposikia kuwa Yesu yupo. 56Kila mahali Yesu alipokwenda, iwe vijijini, mijini na mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni, wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa, waliponywa.

Copyright information for Neno