Mark 9

1Yesu akaendelea kuwaambia, “Amin, amin nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija katika nguvu.”

Yesu Ageuka Sura

2Baada ya siku sita, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao. 3Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko ambavyo mtu ye yote duniani angaliweza kuyang'arisha. 4Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Yesu.

5Petro akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kingine cha Eliya.” 6Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana.

7Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka katika lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu, nimpendaye, msikilizeni yeye.”

8Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine ye yote pamoja nao isipokuwa Yesu.

9Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawakataza wasimwambie mtu ye yote mambo waliyoona, mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuka kutoka kwa wafu. 10Wakalihifadhi jambo hilo wao wenyewe, lakini wakawa wanajiuliza, “Huku kufufuka kwa wafu maana yake nini?”

11Wakamwuliza, “Kwa nini walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?”

12Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya yuaja kwanza, ili kurudisha upya mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa? 13Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu yeye.”

Kuponywa Kwa Mvulana Mwenye Pepo Mchafu

14Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao. 15Mara wale watu walipomwona Yesu, wakastaajabu sana, wakamkimbilia, ili kumsalimu.

16Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”

17Mtu mmoja miongoni mwa ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anamfanya asiweze kuongea. 18Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”

19Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitachukuliana nanyi mpaka lini? Mleteni huyo mvulana kwangu.”

20Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Yesu, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.

21Yesu akamwuliza baba yake, “Mwanao amekuwa akitokewa na hali hii tangu lini?”

Akamjibu, “Tangu utoto wake.
22Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lo lote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”

23Yesu akamwambia, “Kama ukiweza kuamini, yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”

24Mara baba yake yule mvulana akapiga kelele akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!” 25Yesu alipoona kwamba umati wa watu unakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke wala usimwingie tena!”

26Yule pepo mchafu akiisha kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” 27Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua, naye akasimama.

28Baada ya Yesu kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”

29Yesu akawajibu, “Hali hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba na kufunga.”

Yesu Atabiri Tena Kifo Chake Na Ufufuo

30Wakaondoka huko, wakapitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu ye yote afahamu mahali walipo, 31kwa maana alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu nao watamwua, naye siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32Lakini wao hawakuelewa kile alichokuwa akisema, nao waliogopa kumwuliza.

Mabishano Kuhusu Aliye Mkuu Zaidi Ya Wote

33Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?” 34Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao aliyekuwa mkuu zaidi ya wote.

35Akaketi, akawaita wote kumi na wawili akawaambia: “Kama mtu ye yote akitaka kuwa wa kwanza hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”

36Kisha akamchukua mtoto mdogo akamsimamisha katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, 37“Mtu ye yote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo, kwa Jina langu anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”

Ye Yote Asiye Kinyume Nasi Yuko Upande Wetu

38Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako nasi tukamkataza kwa sababu yeye si mmoja wetu.”

39Yesu akasema, “Msimkataze, hakuna ye yote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lo lote baya dhidi yangu. 40Kwa maana ye yote asiye kinyume chetu yuko upande wetu. 41Amin, amin nawaambia, ye yote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Kristo, hakika hataikosa thawabu yake.”

Kusababisha Kutenda Dhambi

42“Kama mtu ye yote akimsababisha mmojawapo wa wadogo hawa wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa afadhali mtu huyo afungiwe shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini. 43Kama mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja kuliko kuwa na mikono miwili ukaingia jehanamu mahali ambako moto hauzimiki. 44[Mahali ambako funza wake hawafi wala moto wake hauzimiki]. 45Kama mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa kilema kuliko kuwa na miguu miwili ukaingia jehanamu mahali ambako moto hauzimiki. 46[Mahali ambako funza wake hawafi wala moto hauzimiki.] 47Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, ling'oe. Ni afadhali kuwa chongo ukaingia katika Ufalme wa Mungu kuliko kuwa na macho mawili na ukatupwa jehanamu, 48mahali ambako “ ‘funza wake hawafi,
wala moto wake hauzimiki.’


49Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.

50“Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”

Copyright information for Neno